Habari za Kitaifa

Shilingi yaimarika thamani yake

February 15th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

SHILINGI ya Kenya mnamo Jumatano iliimarisha thamani yake dhidi ya dola ya Marekani kwa kiwango kikubwa zaidi kwa miaka 12 iliyopita, hali ambayo imetajwa kuongeza imani ya wawekezaji kwa mwelekeo wa kiuchumi nchini.

Kwa siku 11 zilizopita, thamani ya shilingi imeimarika kimiujiza kutoka Sh160 dhidi ya dola moja hadi Sh153.75.

Tangu Novemba 2023, thamani ya shilingi imekuwa ikishuka sana dhidi ya sarafu za kigeni, hali ambayo ilikuwa imeanza kuzua wasiwasi miongoni mwa wawekezaji na mashirika ya kimataifa ya kifedha ambayo huwekeza nchini au kutoa mikopo kwa Kenya.

Kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo, benki ya Equity ilikuwa ikiuzwa dola kwa Sh153.75 huku Benki ya Kenya Commercial (KCB) ikiiuza kwa Sh157.5.

Hata hivyo, vituo vya kubadilishia sarafu vilikuwa vikiuza dola moja kwa kati ya Sh152 na Sh157.

Mnamo Jumanne, Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliweka bei ya wastani ya dola kuwa Sh156.7.

Kulingana na wadasisi wa masuala ya kiuchumi, kuimarika kwa thamani ya shilingi kunatarajiwa kupunguza gharama ya kuingiza bidhaa nchini kutoka mataifa ya nje.

Kwa serikali, hatua hiyo itapunguza mzigo na gharama ya kulipa madeni ya nje.

Kulingana na CBK, mabadiliko madogo tu ya thamani ya shilingi huwa yanaathiri ulipaji madeni kwa karibu Sh40 bilioni.

Hivyo, kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola kwa Sh3.62  kutaipunguzia Kenya gharama ya ulipaji madeni yake kwa Sh144.8 bilioni, kwa muda wa siku nane tu.

Wachanganuzi wanasema kuwa hali hiyo pia inaashiria kuwa kuna idadi kubwa ya wawekezaji wanaorejea nchini.

“Kile kinachofanyika ni kwamba kuna taasisi nyingi za uwekezaji zinazorejea nchini. Hili bila shaka, litaongeza uwepo wa dola nchini, hivyo kupunguza uhaba uliokuwepo,” asema Bw Tony Watima, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kiuchumi.

Wiki iliyopita, Gavana wa CBK Kamau Thugge, alisema kuwa shilingi ilikuwa imepita kiwango cha kushuka kwake, hivyo hawakuwa na hatua nyingine ila kuingilia kati ili kudhibiti usawa wake dhidi ya sarafu za kigeni.

“Ni maoni yangu kwamba kiwango cha ubadilishanaji shilingi kimepita usawa wake. Kuna uwezekano wa kudhibiti ubadilishanaji wake kuanzia sasa,” akasema Dkt Thugge.