Fahamu jinsi ‘airbags’ zinavyofanya kazi kumlinda mwathiriwa wa ajali
Huku watu wengi wakiendelea kupoteza maisha yao kupitia ajali za barabarani nchini, Taifa Leo imezungumza na wataalamu kadhaa kuhusu jinsi kifaa hicho kinavyoweza kumlinda mwathiriwa wakati ajali inapotokea.
Kwanza, mifuko hiyo huwa kifaa muhimu sana kwenye magari tangu kubainika kwake.
Huwa inamlinda mtu dhidi ya kupata majeraha au kuvunjwa sehemu muhimu za mwili ajali inapotokea.
Wataalamu wanasema kuwa mifuko hiyo huwa imetengenezewa madereva na abiria.
Kulingana na mhandisi wa mitambo Gerrishon Mwamburi, watu ambao hawajawahi kupata au kuhusika kwa ajali barabarani hawawezi kufahamu umuhimu wa mifuko hiyo.
Hata hivyo, anaonya kuwa mifuko hiyo pia inaweza kumjeruhi vibaya mtu, endapo itakosa kutumika vizuri.
“Airbags huwa muhimu sana. Tafiti kadhaa zimeonyesha kuwa huwa zinapunguza maafa kwa karibu asilimia 30. Watu wengi wamenusurika vifo kutokana na ulinzi wa vifaa hivyo muhimu. Wengine wamezuiwa kupata majeraha mabaya walipopata ajali. Hata hivyo, kuna umuhimu watengenezaji wake kuboresha miundo yake ili kuimarisha umahsusi wake katika kuwalinda abiria,” akasema Bw Mwamburi.
Mtaalamu huyo anaonya kwamba ingawa ‘airbags’ zimeundwa ili kuwalinda abiria, zinaweza kusababisha madhara, hasa wakati dereva au abiria anapokaa karibu sana nayo.
“Kukaa karibu sana na ‘airbag’ kunaweza kumsababishia mtu majeraha ya kichwa na shingo. Pia, baadhi ya ‘airbags’ zinaweza kuwa na kemikali zinazoweza kusababisha madhara kwa macho au kuleta matatizo ya kupumua mara ajali inapotokea. Katika hali mbaya zaidi, ‘airbags’ pia zinaweza kusababisha majeraha ya akili au sehemu nyingine za ndani za mwili,” akasema Bw Mwamburi.
Je, ni vipi mtu anafaa kutumia airbag?
Kwanza, wataalamu wanasema kuwa lazima mtu akae umbali wa angalau inchi 10 kutoka kwa ‘airbag’ ili kujilinda dhidi ya kupata majeraha mabaya.
Pili, madereva wanashauriwa kuweka mikono yao kwenye usukani–steringi–la sivyo ‘airbag’ inaweza kuigonga inapojaa hewa.
Tatu, wataalamu wanashauri kwamba lazima mtu avae mkanda wa usalama, kwani hili huongeza ulinzi anaopata kutoka kwa ‘airbag’ ajali inapotokea.
Nne, wanashauri kwamba kwa wanawake wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka 12, ni vizuri wakae nyuma ya magari ili kuwalinda na madhara yoyote yanayoweza kuwakumba wakati wa ajali.
“Kwa kuzingatia hayo, bila shaka mtu atajilinda dhidi ya kupata madhara wakati wa ajali,” akasema Bw Mwamburi.