Dalili Raila anastaafu kutoka ulingo wa siasa
Bw Odinga alitoa kauli hiyo Alhamisi, kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.
Bw Odinga alisema kuwa yuko tayari kuhudumu katika nafasi hiyo, ikizingatiwa hapo awali aliwahi kuhudumu kama Mwakilishi wa Ngazi za Juu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundomsingi.
Akiandamana na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, Bw Odinga alisema kwamba ametafuta ushauri wa kutosha kuhusu uamuzi wake.
Bw Obasanjo, kwa upande wake, alimtaja Bw Odinga kama mwaniaji bora kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kujaza nafasi hiyo, inayoshikiliwa na Mahamat Faki kutoka Chad.
Kutokana na tangazo hilo, wadadisi wanasema kuwa huenda hiyo ikawa dalili ya Bw Odinga kujiondoa kutoka ulingo wa siasa nchini, hasa baada ya kuwania urais mara tano bila kuibuka mshindi.
Bw Odinga aliwania urais kwa mara ya kwanza mnamo 1997, chini ya chama chake cha National Development Party (NDP).
Baadaye, aliwania urais mnamo 2007, 2013, 2017 na 2022.
Katika majaribio hayo yote, hajaibuka mshindi, licha ya hata kuwa na uungwaji mkono wa serikali mnamo 2022.
Kulingana na Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw Odinga analenga “kustaafu kiungwana na kwa njia ya utulivu kutoka ulingo wa siasa nchini”.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo , Alhamisi, mdadisi huyo alisema kuwa Bw Odinga anaonelea kazi hiyo ikiwa njia tulivu ya kuepuka shinikizo ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake, kwa mfano “kumrejeshea mkono” kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kwa kumuunga mkono kuwania urais 2027.
“Kwa sasa, Bw Odinga yuko kwenye njiapanda kuhusu nia yake ya kuwania urais 2027. Kwa upande mmoja, baadhi ya wafuasi wake wanasisitiza kuwa lazima awe debeni. Pili, washirika wa Bw Musyoka wanashikilia kwamba lazima amuunge mkono, baada ya kusimama naye 2013, 2017 na 2022. Hilo ni ikizingatiwa mnamo 2022, Bw Musyoka alimuunga mkono licha ya kutomteua kama mgombea-mwenza wake,” akasema Prof Kagwanja.
Wadadisi wanasema kuwa huenda pia kuna mkono wa Rais William Ruto kwenye juhudi hizo, kufuatia ‘handisheki fiche’ iliyofikiwa baina ya Rais na Bw Odinga jijini Mombasa mwaka 2023, chini ya uwepo wa Bw Obasanjo.
Wanaeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba hiyo ni moja ya ahadi ambayo Bw Odinga alipewa, ili kusitisha maandamano ambayo alikuwa akiwaongoza wafuasi wake dhidi ya serikali.
“Bila shaka, kuna uwezekano mkubwa kuwa hii ni moja ya ahadi ambayo Bw Odinga alipewa ili kusitisha maandamano. Haijulikani masuala ambayo viongozi hao watatu walijadili, kwani kikao chao kilikuwa cha faragha,” asema Bw Oscar Plato, aliye mdadisi wa masuala ya kisiasa.
Ikizingatiwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya AU huwa anahudumu kwa jumla ya miaka minne, wadadisi wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa Bw Odinga asiwe debeni 2027, kwani ikiwa ataanza kuhudumu mwaka huu, basi muhula wake utakamilika mnamo 2028.
“Kwa kawaida, Bw Odinga atamaliza kuhudumu kama mwenyekiti wa tume hiyo mnamo 2028. Hivyo, itakuwa vigumu kwake kushiriki kwenye uchaguzi huo. Pili, umri wake utakuwa umesonga sana (atakuwa na umri wa miaka 82). Bila shaka hangependa kuwa katika mazingira ya siasa kali katika umri huo,” akasema.