Habari za Kitaifa

Naibu Rais Rigathi awaonya Wakenya wanaozidi kukwamilia sarafu ya Amerika

February 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewashuari Wakenya wanaomiliki sarafu za Marekani za dola, kuziuza upesi ili kupeuka kupata hasara.

Akizungumza katika eneo la Kandara, Kaunti ya Murang’a, Naibu Rais alihusisha kudorora kwa dola na mikakati kabambe iliyowekwa na bosi wake Rais William Ruto.

Huku akiwahimiza Wakenya kuwa na imani na shilingi ya Kenya ambayo imeanza kupata afueni baada ya kipindi kigumu, Bw Gachagua alikadiria kuwa sarafu ya dola itashuka hata zaidi hadi kufikia 100.

Aidha, Naibu Rais amewaonya Wakenya ambao bado wameshikilia dola kuziuza katika muda wa siku tatu la sivyo, huenda wakapata hasara kubwa.

“Rais amepanga kazi dola imeteremka, imeteremka, sasa wale wako na dola wanakimbia kwa benki kuuza haraka. Kwa leo imeteremka mpaka 137,”alisema Naibu Rais.

“Nataka niwaambie Wakenya kwa sababu ninawapenda acheni niwaibie siri. Huyu Rais vile amepanga hii dola muuze leo, kesho na kesho-kutwa. Msipouza mtaenda hasara kubwa, hii dola mimi naona Rais amepanga itafika 100.”

Kwa mujibu wa Bw Gachagua, baadhi ya Wakenya wameanza kufurika benki kubadilisha sarafu zao za kigeni baada ya shilingi ya Kenya kuandikisha matokeo bora zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa muda mrefu dhidi ya sarafu ya Amerika.

“Wakenya wale wako na dola, jana wamejaa kwa benki, leo asubuhi wako huko. Wale ambao wamebakisha dola mkimbie haraka msiende hasara. Si nimewapa siri wakipoteza wasiniulize mimi,” alisema Bw Gachagua.

Kauli ya Naibu Rais anayefahamika kwa jina la utani Riggy G, imejiri siku moja tu baada ya Shilingi ya Kenya kuongeza thamani yake pakubwa.

Mabadiliko hayo ya hivi punde yameashiria matumaini hasa wakati huu ambapo raia wamelemewa na gharama ya juu ya maisha ikiwemo bei ghali za vyakula na bidhaa za kimsingi.

Hata hivyo, kuimarika ghafla kwa shilingi yaa Kenya dhidi ya sarafu ya Amerika kumeibua hisia mseto huku baadhi ya Wakenya wakitilia shaka na kusisitiza kusubiri kwa muda ili kuthibitisha.

Mnamo Alhamisi, thamani ya Shilingi ya Kenya iliruka hadi kufikia 145 dhidi ya sarafu ya Amerika kutoka 167.

Wafanyabiashara na watoaji huduma wanaolipwa kwa kutumia sarafu ya dola hata hivyo, wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na misukosuko kwenye soko la hisa wakihofia kupata hasara.