Jamvi La Siasa

Gachagua alivyomshushia Nyoro makombora siku ya mwisho ziara ya Rais Mlimani

February 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

STEPHEN MUNYIRI NA LABAAN SHABAAN

MAKABILIANO ya ubabe kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro yanaendelea licha ya harakati za kupoza uhasama wa kisiasa kuendelea.

Naibu Rais amemwita Mbunge wa Kiharu mtalii wa kisiasa akiwataka viongozi wachanga wakome kujinadi kisiasa msimu usio wa kampeini.

Haya yanajiri licha ya mwito kutolewa kwa wawili hao kutuliza makabiliano yanayolemaza mpango wa kuunganisha viongozi wa eneo la Mlima Kenya.

Naibu Rais, aliyeandama na Rais William Ruto, alimrushia cheche Bw Nyoro alipozungumza akiwa eneobunge la Mathira Ijumaa.

“Huu si wakati wa mabishano ya kisiasa yanayolenga kusababisha utengano katika eneo letu lakini kampeini zikianza, tuko tayari kwa wanaotupinga,” alisema kisha akamkaripia Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi.

“Kwa sababu wewe ni wa hapa (Mathira), kaa nyumbani na usiwafuate watalii wa kisiasa wanaozurura kote nchini. Hatufai kukubali kutenganishwa kwa vile umoja wetu ndio nguvu yetu.”

Mwezi mmoja uliopita kundi la wabunge kutoka maeneo mbalimbali nchini lilimuunga mkono Bw Nyoro kuwa Rais mwaka wa 2032 ‘badala ya Bw Gachagua.’

Baada ya siasa za ubabe kutokota, baadaye Mbunge wa Kiharu alionekana kupuuza uhasama huu kwa kusema anawaunga mkono Rais na Naibu Rais.

Utalii wa kisiasa unaakisi tukio la miaka ya themanini ambapo aliyekuwa Rais marehemu Mwai Kibaki (akiwa Makamu wa Rais mwendazake Daniel Moi)  alimkabili Waziri Elijah Mwangale ambaye alikuwa anashinikiza kubanduliwa kwa Bw Kibaki.

Rais wa awamu ya tatu, Mwai Kibaki, alimkaripia Bw Mwangale akimwambia akome siasa za utalii zilizolenga kumharibia mpango wa kurithi uongozi kutoka kwa Rais Moi.