Baada ya ‘Yesu Ninyandue’, fahamu nyimbo nyingine za ‘injili’ zilizozua utata
NA WANDERI KAMAU
BAADA ya utata kuzuka kuhusu wimbo ‘Yesu Ninyandue’ wake mwimbaji William Getumbe kutoka Kanti ya Uasin Gishu, imeibuka kuwa si mara moja utata kama huo kuhusu nyimbo zilizotajwa kuwa za ‘injili’.
Darubini ya Taifa Leo inarejea nyuma na kuangazia nyimbo ambazo zishawahi kuzua utata kutokana na jina au jumbe zake kanganyishi.
Mnamo 2016, mwanamuziki Jimmie Gait alijipata matatani, baada ya kutoa wimbo ‘Yesu Ndiye Sponsor’.
Wimbo huo ulizua midahalo na hisia kali miongoni mwa Wakristo, walioutaja kuwa “kejeli kwa Mwenyezi Mungu”.
Ijapokuwa Gait alijaribu kujitetea, akifafanua maana kamili ya wimbo huo, mashabiki wake walionekana kutomsikiliza.
Kwa wakati mmoja, alibubujikwa na machozi kwenye runinga, akielezea jinsi watu walivyosahau nyimbo nzuri ambazo alikuwa amewaimbia hapo awali.
Mnamo 2017, mwanamuziki SBJ alizua gumzo nchini, baada ya kutoa kibao ‘Yesu Nipe Nyonyo.’
Kama Jimmie Gait, mwanamuziki huyo alijaribu kuelezea maana ya wimbo huo, akisema alimfananisha Yesu na chemichemi ambapo watu hupata shibe.
Hata hivyo, Wakenya walimkosoa vikali, baadhi wakizishinikiza taasisi za serikali zinazosimamia miziki kuupiga marufuku na mwanamuziki husika kukamatwa.
Kwa mwanamuziki Willy Paul, si mara yake ya kwanza kujipata matatani, kwa kuimba nyimbo zilizofasiriwa kutokuwa na maadili ya Kikristo.
Mnamo 2013, alijipata matatani baada ya kutoa wimbo ‘Missi’. Baadhi ya mistari ya wimbo huo ilieleza “Mwenyezi nimekumissi sana…”
Hata hivyo, baadhi ya Wakristo walimkosoa mwanamuziki huyo, wakiutaja wimbo huo kuwa kejeli kwa Mungu.
Nyimbo zake nyingine ambazo zimekumbana na ukosoaji huo ni kama ‘Mpenzi’, ‘Take it Slow’ na ‘Tiga Wana’.
Kwenye wimbo mpenzi, mwanamuziki huyo anamfananisha Yesu na mpenzi wake, akisema kwamba [Yesu] huwa anamsaidia katika nyakati zote.
Wimbo ‘Take it Slow’ nao ulikuwa “onyo” kwa watu kuhusu athari za kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi ovyo ovyo.
Kwenye wimbo ‘Tiga Wana’ (Acha Ujinga), Willy Paul alisema kwamba alitoa ujumbe huo kama “onyo kwa Shetani kutomletea mchezo kwani angempiga kwa nguvu za maombi na Roho Mtakatifu”.
Katika siku za hivi karibuni, mwanamuziki Embarambamba ndiye amekuwa akizua midahalo kwa kutoa nyimbo zinazotajwa kuwa kejeli kwa injili, kama vile ‘Nataka Kunyonywa’, ‘Imesimama’, ‘Napenda Mbele, Sipendi Nyuma’ kati ya nyingine.
Amekuwa akisisitiza kuwa watu wamekuwa wakizifasiri vibaya.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Kusimamia Muziki Kenya (MCSK), Dkt Ezekiel Mutua, anasisitiza kuwa lazima wanamuziki wazingatie maadili wanapotunga nyimbo zao.