Makala

Jifunze namna ya kutumia jiwe la kusaga unga kitamaduni

February 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA KALUME KAZUNGU

KATIKA ulimwengu wa leo, nafaka zimekuwa zikipondwa na kisha kusagwa na kuwa unga kupitia mbinu za kisasa, ikiwemo matumizi ya mtambo wa kusaga nafaka au kwa jina lingine kinu.

Mtaani wengi wanaita mtambo huo wa kisasa ‘kisiagi’.

Matumizi ya mashine au kinu kuponda au kutwanga nafaka, ikiwemo mahindi, mtama, mawele, na wimbi yamerahisishwa si haba katika karne hii ya 21, ambapo mitambo mingi hutumia umeme, dizeli au petroli kutekeleza jukumu hilo.

Usichokijua ni kwamba zama za kale au enzi za mababu zetu, vyombo vya kisasa kama mtambo wa kusagia havikuwepo.

Mababu zetu walikuwa wakitumia mbinu za jadi kutwanga au kusaga mahindi na nafaka nyingine ili kujipatia unga wa kuandaa mlo kama vile ugali, chapatti, mkate wa sinia, vitumbua nakadhalika.

Taifa Leo ilizama chini kuchunguza na kuchanganua namna ya kutumia jiwe la kusaga unga kitamaduni.

Kwanza, mawe yenyewe ya kusaga nafaka kuwa unga yalikuwa ya aina au maumbo tofautitofauti ilmradi watumiaji wawe na ujuzi wa kutumia aina hizo za mawe katika kuafikia aina ya unga waliyohitaji.

Taifa Leo ilifafanua mojawapo ya jiwe la kusaga unga kitamaduni ambalo ni la aina ya mviringo au duara.

Ili kupata unga kwa mfano ule wa mahindi, mtengenezaji kwanza huhitajika kutumia kinu cha kiasili ambacho sio ule mtambo wa kusagia mahindi.

Kinu hiki cha kiasili, ambacho hadi wa leo pia kinatumika miongoni mwa jamii, hasa zile zinazoishi maeneo ya mashambani, ni chombo kama mtungi kilichoundwa kutokana na gogo.

Mahindi hapa huingizwa ndani na kisha kutwangwa kwa kutumia mti uitwao mchi.

Hatua hii hutekelezwa kwani azma kuu huwa ni kubambua maganda ya nje ya nafaka au wishwa, hasa mahindi.

Baadaye mahindi hutandazwa mkekani na kisha kuanikwa juani hadi kukauka vizuri na kisha kuanza kusagwa kwa kutumia jiwe hilo la mviringo.

Lakini je, jiwe hili likoje?

Ifahamike kuwa mawe mawili yaliyo na ukubwa sawa huchongwa umbo sawa la mviringo kama magurudumu.

Kisha jiwe moja huwekwa chini ilhali lingine likimlalia mwenzake kwa upande wa juu.

Jiwe la chini, ambalo ndilo mama, hutobolewa kitundu kidogo katikati, ambapo kijiti imara huingizwa na kuhakikishwa kimesimama tisti.

Jiwe la juu nalo hutobolewa au kuchongwa tundu pana ya mviringo katikati.

Kisha kuna sehemu ya karibu na mwisho wa jiwe hilo la juu ambapo pia hutobolewa kitundu kingine kinachoingizwa kijiti.

Kijiti hicho ndicho kinachotumika kama mpini wa kuzungushia jiwe hilo la juu wakati shughuli ya kutengeneza unga inapoanza.

Ifahamike kwamba jiwe la chini (jiwe-mama) huwa halizungushwi bali husalia tisti hivyo wakati maandalizi ya unga yanapofanyika.

Waandalizi wa unga kitamaduni huanza kwa kutandikia mawe haya mkeka maalumu wa kusagia.

Kisha huchukua jiwe-mama na kuliweka katikati ya kitandiko au mkeka husika.

Hatua ya pili ni kuchukua jiwe la pili na kulikalisha juu ya jiwe hilo mama, ambapo kijiti kilichotundikwa kwenye jiwe la kwanza lililoko chini hupitishwa katikati ya tundu pana iliyochongwa.

Baadaye watengenezaji unga, mara nyingi wakiwa ni akina mama, hujibanza kandokando ya jiwe na kuanza kuzungusha kwa mikono ilhali wakiingiza nafaka kwenye mawe hayo kupitia tundu pana ya jiwe la juu na kuipondaponda.

Utapata kwamba kila wanapoingiza nafaka na kuzungusha jiwe la juu, unga au vipande vidogo vidogo vya nafaka huanza kujitokeza pembezoni mwa mawe hayo na kudondoka kwenye mkeka maalum wa kusagia.

Inategemea ni unga wa nini mtengenezaji analenga kuandaa.

Ikiwa ni unga wa chenga nyepesi, utahitajika kuingiza nafaka mara ya kwanza kuzungusha jiwe.

Kisha utazoa tena vipande au unga ulioandaa au kudondoka mkekani raundi ya kwanza na kuurudisha tena kwenye mawe kuendelea kuusaga mara kadhaa hadi uwe na chenga nyepesi kabisa.

Punde hili likiafikiwa, kuna wengine ambao huutumia unga moja kwa moja ilhali baadhi huuweka unga huo kwenye uteo na kuupepeta kutenganisha magamba au wishwa ambao huenda haukusagika vizuri, hivyo kupata unga laini kabisa wa kupikia sima au ule wa chenga za kuandalia mkate, uwe ni wa sinia au vitumbua.

Kwa wale wasiofahamu, jiwe hili la kusagia linaweza kuviringishwa na mtu mmoja au wawili kwa wakati mmoja ilmradi wasichoke haraka kusaga unga.

Utapata akina mama wawili, mmoja amekaa upande huu na mwingine upande ule, ambapo husukuma jiwe kwa ustadi na kuandaa unga mwingi.

Jiwe hili la kusagia kwa muda mrefu limekuwa likitumika na jamii mbalimbali za Kenya na bara zima la Afrika.

Baadhi ya jamii zinazotumia jiwe hilo la kusagia ni Wamijikenda, ikiwemo Wagiriama, Waduruma na wengineo.

Jamii ya Waswahili wa asili ya Wabajuni pia imekuwa ikitumia sana jiwe hili katika kuandaa unga wa kutayarishia mlo, hasa mkate wa sinia, vitumbua na uji.

Mbali na kuandaa unga, jiwe la kusagia pia lilisaidia kuleta umoja na ukarimu miongoni mwa jamii nyingi, hasa zile za mwambao wa Pwani.

Utapata akina mama wa familia mbalimbali wakija pamoja na kushirikiana kuandaa unga kienyeji kwa kutumia jiwe la kusagia.

Bi Mwanasiti Said anasema ushirikiano uliokuwepo wakati wa kutengeneza unga kupitia jiwe kitamaduni ulikuwa na tija ya chakula kuandaliwa kwa pamoja na kisha watu kukaa pamoja kufurahia mlo.

Bi Mwanasiti Said akionyesha umaridadi katika kusaga na kutayarisha unga kitamaduni Lamu. Jiwe la kusagia limekuwa likitumika tangu jadi katika kusaga nafaka. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Said anakejeli mbinu za sasa za kusagia unga (nafaka), ambapo watu wengi wameibukia matumizi ya mashine, hivyo kuleta tabia ya uchoyo miongoni mwa jamii au familia.

“Ukitazama hakuna tena ushirikiano kama awali ambapo sisi wamama tungekuja pamoja kusaga unga tukitumia jiwe la kusagia na kisha kuandaa mlo utakaoliwa na wengi. Leo kila mtu kivyake. Wengine hata wako na mashine za kusagia majumbani mwao. Wanaandaa vyakula na kula kichoyo bila ya kuangalia wengine. Ni Dhahiri mbinu za sasa za kutayarisha unga zimepelekea kusheheni kwa uchoyo katika jamii,” akasema Bi Said.

Zainab Ahmed, mtaalamu wa lishe kisiwani Lamu, anawahimiza wakazi kuendelea kutumia mbinu za zamani za kuandaa au kusaga nafaka, akizitaja kuwa muhimu zaidi kwa afya yao.

“Mimi mwenyewe napendelea sana kusagiwa unga au nafaka kwa kutumia mbinu za kienyeji kama jiwe la kusagia kuliko mashine. Unga unaosagwa na mashine hupitishwa kwenye awamu tofautitofauti ambazo ninaamini zinaondoa madini muhimu chakulani. Kusaga unga kienyeji utapata nyuzinyuzi muhimu kwa usagaji wa chakula mwilini zikiachwa. Mashine za kisasa zinapoandaa unga huchuja nyuzinyuzi hizo,” akasema Bi Ahmed.

Wazungu wakitumia kinu kuponda mahindi kisiwani Lamu. Kinu ni miongoni mwa vifaa vinavyotumiwa kuandalia unga, hasa ule wa mahindi kienyeji. PICHA | KALUME KAZUNGU