Habari za Kitaifa

Raila apigwa jeki na Azimio, Serikali AUC

February 17th, 2024 2 min read

MOSES NYAMORI NA VICTOR RABALLA

VINARA wa Azimio la Umoja-One Kenya wakiongozwa na kigogo wa Wiper Kalonzo Musyoka wameunga mkono hatua ya kiongozi wao Raila Odinga kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) huku wakiahidi kudumisha umoja katika mrengo huo wa upinzani.

Haya yanajiri huku ikiibuka kwa Rais William Ruto amekuwa akiendesha kampeni za kisiri miongoni mwa Marais wa Afrika za kumpigia debe Odinga kwa cheo hicho nyakati za ziara zake nje.

Duru zimeambia Taifa Leo kwamba kampeni hizo za Dkt Ruto zimekuwa zikipigwa jeki na aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo tangu mwaka jana alipoongoza maridhiano kati ya wawili hao yaliyozima maandamano dhidi ya serikali.

“Hii ndio maana Bw Obasanjo aliandamana na Raila wakati kiongozi huyo wa Azimio alipotangaza rasmi kwamba atawania cheo hicho. Na dakika chache baadaye Rais huyo wa zamani wa Nigeria akafululuzi hadi Murang’a kukutana na Rais,” akasema afisa mmoja wa cheo cha juu serikalini ambaye aliomba tulibane jina lake.

Akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi mnamo Ijumaa, Bw Musyoka ambaye alikuwa ameandamana na wenzake Eugene Wamalwa, Jeremiah Kioni, George Wajackoyah na Peter Munya aliahidi kuwa atajiunga na kikosi cha kumfanyia kampeni Bw Odinga kote Afrika.

Duru zinasema kuwa kikosi hicho kitaongozwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye pia ndiye anasimamia Wizara ya Masuala ya Kigeni.

“Kama kiongozi mwenye tajriba kubwa katika masuala ya diplomasia na kwa kuwa nimehudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni kwa muda, na Makamu wa Rais ninaamini kuwa Odinga atapata uungwaji mkono mkubwa kote Afrika. Binafsi nitakuwa mstari wa mbele kumpigia debe katika mataifa yote 54 wanachama wa Umoja wa Afrika,” Bw Musyoka akaeleza.

“Sisi katika Azimio tunampa kiongozi wetu baraka zetu zote na kumhakikishia kuwa mrengo wetu utasalia na nguvu hata akiondoka na kujikita kwenye kibarua hicho cha hadhi endapo atashinda kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu,” Bw Musyoka akaongeza.

Lakini huku Bw Odinga akionekana kupata uungwaji mkono kutoka serikali ya Kenya na mrengo wake wa upinzani, imeibuka kuwa amepata upinzani kutoka ukanda wa Afrika Mashariki yenye mataifa manane.

Duru zinasema mbunge mmoja wa zamani nchini Sudan Kusini, ambaye jina lake halikufichuliwa moja, amejitoza ulingoni kuwania kiti hicho. Aidha, inasemekana kuwa mwaniaji mwingine anatoka katika taifa la Nigeria.

Bw Odinga alihitaji uungwaji mkono mkamilifu kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili awe katika nafasi bora wa kupata ushindi wa rahisi.

Hata hivyo, kamati ya serikali itakayompigia debe Bw Odinga imeapa kushawishi mataifa hayo yote kumchagua kiongozi huyo wa Azimio ili ajaze nafasi ambayo itasalia wazi baada ya mwenyekiti wa sasa Moussa Faki Mahamat kustaafu baadaye mwaka huu 2024.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama wa Wafanyakazi Nchini (Cotu) Francis Atwoli ameunga mkono azma ya Bw Odinga kuwania wadhifa huo.