Habari za Kaunti

Uuzaji, usafirishaji makaa wadhibitiwa vikali Pokot Magharibi

February 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

NI marufuku kufanya biashara ya kuuza na kusafirisha makaa zaidi ya gunia moja kutumia pikipiki na magunia matatu kutumia gari katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Haya ni kulingana na notisi iliyotolewa mwishoni mwa Januari 2024.

Akiongea na Taifa Leo, Afisa Mkuu wa Maji, Mazingira, Maliasili na Masuala ya Tabianchi katika Kaunti ya Pokot Magharibi Leonard Kamsait alisema kuwa ni hatia kuuza makaa kwa kiwango kikubwa.

Notisi hiyo vilevile inawataka wote wanaonuia kusafirisha mbao na miti kutafuta leseni kutoka idara ya mazingira na pia wanaofanya matangazo ya kibihashara kutumia vipaza sauti kukata leseni kutoka idara hiyo ya mazingira kama njia mojawapo ya kudhibiti kero kwa mazingira.

“Hakuna mtu anayeruhusiwa kuuza ama kubeba makaa kiasi kingi,” alisema Bw Kamsait.

Mtaalamu wa usimamizi wa maliasili kutoka shirika la World Vision Lavender Ondere alisema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuonekana wazi.

“Ni jukumu la kila mtu kuhusika kwenye mchango huu Tutafanya kazi na mashirika tofauti na serikali ya kaunti,” alisema Bi Ondere.

Alisema kuwa wako na mpango wa kupanda miti kwenye shule ili kusaidia jamii kurejesha mfumo wa ardhi.

“Miti iko na umuhimu wake wa kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuleta mvua,” alisema.

Bi Ondere alisema kuwa mipango ya shirika hilo inahusu kuweka miche ya miti kwenye nasari.

Alisema kuwa watasaidia akina mama na vijana kuhusika kwenye shughuli hiyo.

“Ukiangalia vyema kwenye mazingira, jamii itatumia rasilimali ambazo hutoka kwenye mazingira kuinua maisha yao,” alisema afisa huyo.

Alisema kuwa wanalenga maeneo kame ya kaunti ya Pokot Magharibi na yale yameharibiwa na maporomoko ya tope kuzuia kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya anga kama suluhu la kudumu kwa majanga.

“Tumejitahidi kama nchi kupata asilimia kumi ya misitu,” alisema.

Gavana wa Pokot Magharibi Simon Kachapin anasema kuwa wameanzisha kampeini ya kuongeza idadi ya misitu hadi asilimia 10 na zaidi katika kaunti hiyo.

Gavana huyo aliwahimiza wakulima na taasisi mbalimbali kupanda miti mingi akisema kuwa idara yake itatoa usaidizi wa kitenolojia kwa wale wanaopanda miti katika kaunti hiyo.

“Wakulima wote, watoto, vijana na shule zinaombwa kupanda miti mingi ili kuongeza kiwango cha misitu katika kaunti yetu,” alisema Bw Kachapin.

[email protected]