Afya na Jamii

Kila mara nahisi mkojo hauishi kwenye mrija!

February 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Mpendwa Daktari,
Mimi hutingisha uume wangu baada ya kukojoa ilhali kila wakati mimi huhisi kana kwamba mkojo umesalia. Je tatizo laweza kuwa nini?

Major, Nairobi

Dkt Flo akujibu:
Tatizo la kutiririka kwa mkojo baada ya kukojoa linajulikana kama post micturition dribble.

Hali hii huwakumba wanaume wengi kwa sababu wakati wa kukojoa mrija unaopitisha mkojo (urethra), kwa kawaida hujipinda na huenda mkojo kidogo ukasalia ndani na kutiririka baadaye.

Njia ya kipekee ya kukabiliana na tatizo hili ni kujipa muda unapokojoa ili mkojo uliosalia utiririke.

Aidha, fanya mazoezi ya nyonga ili misuli ya sehemu hii iwe thabiti na iweze kusukuma mkojo nje.

Ili kufanya hivyo, nywea misuli ya nyonga kana kwamba unasitisha mtiririko wa mkojo.

Unaweza kufanya mazoezi ili kutambua misuli fulani kwa kusitisha mkojo katikati ya mtiririko unapokojoa.

Nywea misuli hii kwa takriban sekunde kumi mara kumi wakati mmoja, kati ya mara sita na mara kumi kwa siku.