Habari za Kitaifa

Shinikizo mpya Mt Kenya zataka Uhuru apewe kazi ya AU badala ya Raila

February 19th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KAMPENI ya Rais William Ruto kutaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) zinakabiliwa na dalili za uasi katika eneo la Mlima Kenya, baadhi ya viongozi wa eneo hilo wakipendekeza aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kwa wadhifa huo.

Seneta wa Kaunti ya Kiambu Bw Karungo Thang’wa amekuwa akishinikiza Naibu Rais Rigathi Gachagua kufikiria upya msimamo wa eneo la Mlima Kenya na kumpigia debe Bw Kenyatta kwa wadhifa huo.

Serikali—ambayo kawaida huzungumza kwa sauti moja—imetangaza kwamba inamuunga mkono Bw Odinga kwa wadhifa huo ambapo akifaulu atahudumu kutoka jijini Addis Ababa, Ethiopia hadi 2028, mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 nchini Kenya.

Bw Thang’wa sasa anahisi kwamba Mlima Kenya haukufanyiwa haki na sasa anamuomba Bw Gachagua kuchunguza upya msimamo wa Mlima Kenya kuhusu suala hilo.

“Mimi binafsi sielewi ni kwa nini tunapaswa kumuunga mkono mtu huyo wakati tuna Bw Kenyatta wetu hapa na ambaye pia amehitimu. Hili ni jambo tunalohitaji kujiuliza na kurekebisha ipasavyo,” alisema.

Aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi alisema “Bw Kenyatta kama mkuu wa zamani wa serikali ndiye aliyefaa zaidi na anapaswa kuwa chaguo la Mlima Kenya kama suala la masilahi”.

Alisema mjadala huo ulianzishwa baada ya kampeni za chinichini na ambazo Bw Kenyatta hakufikiriwa kimakusudi.

“Tutamuuliza Bw Kenyatta faraghani iwapo angependa (kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika). Yeye ni mtu mkweli na atatujibu kwa uaminifu. Anastahili. Angekuwa chaguo langu,” alisema.

Msimamo wa Bw Thang’wa unakuza mbegu ya uasi katika Mlima Kenya ambayo imekuwa ikijaribu kuchipuka lakini Rais William Ruto na Gachagua wamechukua hatua za kuzima.

Mshirika wa karibu wa Rais Ruto alidokezea Taifa Leo kwamba Bw Gachagua alikuwa amejaribu kutaja jina la Bw Kenyatta kwa wadhifa huo.

“Bw Gachagua alikuwa amesema kwamba hatua ya kumshawishi Bw Kenyatta kuchukua nafasi hiyo ingeunganisha eneo la Mlima Kenya lakini aliambiwa na rais kuzingatia suala pana la kukabiliana na upinzani mkali zaidi unaoweza kutishia kuchaguliwa kwao tena 2027,” akasema.

Aliongeza kuwa “rais na washirika wengine kadhaa katika muungano tawala walishikilia kauli moja kwamba Mlima Kenya unataka kuonekana kila wakati kushika mateka wengine kila wakati fursa inapotokea na hivyo kufanya hisia za kupinga serikali kuwa kali zaidi”.

Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi Kang’ara aliambia Taifa Leo kwamba Bw Thang’wa anazua hoja ya maana katika mjadala wake.

Jumatatu Februari 19, 2024, Rais Ruto aliongoza wabunge wa Kenya Kwanza kuunga azma ya Bw Odinga kuchaguliwa mwenyekiti wa Odinga akisema ni ushindi kwa Kenya.

Ingawa suala hilo halikuwa sehemu ya ajenda za warsha ya pamoja ya Maafisa wa Serikali ya Kitaifa na wabunge wa muungano tawala huko Naivasha, kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wa alisema Bw Odinga alikuwa na haki ya kuwania wadhifa huo.

“Mkenya anapoteuliwa au kuomba kazi popote ulimwenguni, sisi kama Wakenya tunafaa kumuunga mkono. Haendi huko kama kiongozi wa ODM lakini kama Mkenya na tunaunga azma yake,” alisema Ichung’wa.