Ugali wa Kenya ulivyovutia mgeni kuwekeza kwenye biashara ya viatu nchini
NA SAMMY WAWERU
VINCENT Ndayishemeze, ni kijana barobaro raia wa Burundi ambaye amekuwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja.
Ni mfanyabiashara, japo wa mapato ya chini na ya kadri anayehoji akipewa fursa kwa mara nyingine kuchagua taifa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambalo anaweza kuteua, Kenya itaongoza katika orodha yake.
Ni mchuuzi wa viatu katika Kaunti ya Nairobi, biashara anayohoji aliianza miaka minane iliyopita – akiwa Burundi.
“Niliingilia biashara nikiwa mchanga kiumri. Ninaipenda sana,” Ndayishemeze, 25, anasema.
Tunakutana katika mtaa maarufu wa Roysambu, Nairobi ambako ni ngome yake.
Kwa kawaida, akiwa gangeni huwa na jozi kadhaa za viatu anavyowekelea begani na stoku nyingine kwenye begi (mkoba) mgongoni.
Aidha, huuza viatu maridadi vya mtumba vya wanaume.
“Hubeba idadi ninayoweza, viatu vingine ninaviacha kwenye nyumba,” anadokeza.
Ni barobaro mcheshi, mkwasi wa heshima na mkarimu ambaye ukitangamana naye hata ikiwa hutamudu, utaahidi kumpromoti wakati mwingine kwa sababu ya lugha yake kibiashara.
Hata ingawa hajaafikia malengo yake, anashukuru Mungu kwa hatua alizopiga akiamini wakati mmoja huenda akamiliki duka la kijumla.
Anafichua kwamba ilimgharimu mtaji wa Sh3, 000 (sawa na BIF 60, 000 thamani ya pesa za Burundi) kuanza uuzaji wa viatu, akisema Kenya alijipata kupitia mfanyabiashara wa bidhaa za kijumla za plastiki.
“Tulikutana akijia bidhaa Burundi, akanifumbua macho,” asimulia.
Mengine kama wasemavyo wahenga, yamekuwa historia kilichomvutia zaidi kikiwa ugali wa Kenya.
Kwenye mahojiano na Akilimali, Ndayishemeze alisema alipouonja kwa mara ya kwanza uligeuka kuwa mnato kwake, “hali iliyokaza nati yangu ya mtazamo kusalia Kenya”.
“Kabla kuanza majukumu ya siku, sikosi kumega vipande kadhaa kuongeza nguvu kuchuuza viatu,” aelezea.
Ni kipenzi zaidi akiula kwa kitoweo cha nyama, hasa mbuzi, samaki na omena, mboga akiridhia sukuma wiki na za kienyeji.
Ndayishemeze anasema siku huanza kwa kutua katika soko maarufu la Gikomba, Jijini Nairobi ambapo hununua viatu kwa bei ya jumla.
Kwa kuwa ni viatu vya mtumba, huving’arisha na kuvipiga rangi.
Bei yake ikichezea kati ya Sh1, 000 hadi Sh5, 000 anadokeza kwamba kwa siku hakosi kuuza hadi jozi tatu, siku ikiwa mbaya anachuuza jozi moja.
“Mauzo yakiwa bora zaidi huchuuza hata jozi saba, japo kuna siku ambazo hukosa – nazo ni nadra.”
Masoko yake, hulenga vilabu na baa hususan nyakati za jioni.
Akiwa na matumaini kupanua biashara yake, tangazo la Rais William Ruto 2023 kuifanya Kenya kuwa nchi Viza huru ili kuvutia wawekezaji zaidi na watali linampa matumaini ipo siku ataingia kwenye orodha ya wafanyabiashara tajika.
Akiangalia ukurasa wake wa mafanikio chini ya muda wa mwaka mmoja pekee nchini, Ndayishemeze anahimiza vijana wenza kutoa mikono kwenye mifuko na badala yake wajitume kufanya kazi “hata ikiwa ni kama hii yangu ya juakali isiyopendwa na wengi ilhali ina mapato”.