Mutua, Itumbi watiana makucha kuhusu malipo ya wanamuziki
NA FRIDAH OKACHI
VITA vya usimamizi wa umiliki wa muziki nchini vinazidi kuongezeka. Hivi punde, msimamizi wa mikakati ya kidijitali katika Ikulu Dennis Itumbi na afisa mkuu mtendaji wa chama cha kusimamia muziki Kenya (MCSK) Daktari Ezekiel Mutua wamerushiana cheche za maneno kwenye mtandao wa X (almaarufu Twitter).
Bw Itumbi amemlaumu Bw Mutua kwa matumizi mabaya ya hela za wanamuziki ambao hupokea malipo duni kila mwaka baada ya kusajili na kulipia umiliki wa kazi zao.
Mpango huo, pia unalenga kuwasaidia wasanii kufuatilia mapato yao kwa wakati halisi na kupata malipo yao yote yanayostahili kwa kazi zao za ubunifu.
“…yaani, tunalipa wanamuziki malipo duni na wanalipa mamilioni ya pesa kwa mwaka. Afisa Mkuu Mtendaji wa chama cha kusimamia muziki Kenya analipwa Sh1.3 milioni kwa mwezi. Hii apana! Wacha tuwawezeshe wasanii wetu, kwa hilo, kama vile Paulo katika maandiko, macho yangu yako kwenye mstari wa kumalizia kabisa!” aliandika Bw Itumbi.
Awali Daktari Mutua alilaumu serikali ya Kenya kwanza kwa kutumia eCitizen kukusanya mirabaha, akisema hatua hiyo ni kuingilia usimamizi wa umiliki wa muziki kama mali ya kibinafsi.
“Serikali inafaa kuunga mkono umiliki na mali binafsi ya wanamuziki kwa utekelezaji na kutunga sera sahihi za kulinda. Biashara ya muziki duniani inaendeshwa binafsi kwa sababu serikali haiwezi kufanya biashara nzuri. Kwa hakika, serikali hii tayari imeshatangaza nia yake ya kubinafsisha mashirika ili kupata faida zaidi. Kwa hivyo itakuwa ni mkanganyiko na kuingiliza biashara ya muziki,” alisema Bw Mutua.
Lakini Bw Itumbi alimtaka afisa huyo wa muziki nchini kuelekea mahakamani iwapo si sawa.
“Jiandae kwa eCitizen. Ndiyo unayo haki ya kwenda mahakamiani, lakini wanamuziki wana haki ya kupata mapato moja kwa moja kwa kazi yao ya ubunifu… Jukwaa la kidijiti litakuwa CMO. Tutalinganisha ndoto hiyo ya kidijitali na sheria. Yote yanalenga wasanii,” alisisitiza Bw Itumbi.
Hata hivyo, Bw Mutua alimkashifu Itumbi, akisema kuwa leseni kutoka kwa serikali kwenda kwa CMOs sio upendeleo.
“Hilo haliifanyi Serikali kuwa sehemu ya utawala. Unapingana na jambo hili na utaishia kumwaibisha Rais.”