• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Mabinti Wakenya wanaingia UG ili kukeketwa – Mashirika

Mabinti Wakenya wanaingia UG ili kukeketwa – Mashirika

Na OSCAR KAKAI

MASHIRIKA ya kukabiliana na visa vya ukeketaji katika kaunti ya Pokot Magharibi yamelalamika kuhusu wasichana wengi kuhamia nchi jirani ya Uganda kukeketwa wakati huu wa msimu wa Krismasi.

Uchunguzi wa Taifa leo umeibaini kuwa wasichana wengine huhepa makwao na kuenda kaunti jirani ya Turkana pamoja na nchi jirani ya Uganda ili kukeketwa.

Akiongea Jumapili baada ya wiki moja ya kutoa mafunzo kwa vijana 450 wenye umri wa miaka kati ya 13-18 ambao walifuzu njia mbadala ya kuvuka rika, mshirikishi wa shirika la World Vision, Bw Titus Kaprom, alisema licha ya visa vya ukeketaji kupungua, bado vimeshamiri katika kaunti ndogo za Pokot Kaskazini na Kati.

Alisema kuwa wamejumuisha wavulana kwenye mpango huo ili wajue umuhimu wa kuoa msichana ambaye hajakeketwa.

“Sisi huwapa mafunzo ya kuwalea na kuelekeza ili kubadilisha tabia kutoka Januari, Agosti na Desemba. Tunahakikisha kuwa wanapinga maovu hayo kwa kuwafuatilia. Wengi wao ni wanachama wa vikundi vya mbinu za maisha shuleni,” akasema.

Bw Kaprom alisema kuwa wakazi wamebadilisha mbinu za zamani za kuandaa sherehe na sasa hufanya ukeketaji kisiri.

“Katika maeneo kama Orwa na Marich visa vya ukeketaji ni asilimia 75%, eneo la Sook vimepungua kutoka asilimia 84 hadi 69 huku maeneo kama Masol na Kasei katika kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini viwango bado viko juu,” alisema.

Alisema kuwa shirika hilo limewapa mafunzo zaidi ya vijana 3000 kwenye mpango huo kwa miaka ambayo imepita kuhusu maisha mazuri kuhusu utamaduni bora na mafunzo ya Biblia Takatifu jinsi ya kuepuka ukeketaji.

“Wavulana na wasichana wamepewa stakabadhi na tumewaweka kwenye kumbukumbu zetu.

Bw Kaprom alitoa wito kwa serikali ya kaunti hiyo kushirikiana na mashirika ya kijamii kupigana na ukeketaji katika eneo hilo.

“Visa hivi vimeshamiri msimu huu ingawaje vimepungua kutoka asilimia 100 hadi asilimia 74 na katika maeneo mengine kutoka asilimia 84 hadi asilimia 69. Bado tuko na changamoto kwenye mipaka ya nchi ambapo wasichana huhepa na kuenda kwa watu wa ukoo wao kukeketwa ,”alisema .

Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto alilalamika kuhusu mashirika gushi ambayo yanadanganya kuwa hupigana na visa hivyo katika kaunti hiyo.

“Visa hivyo ni hatari na huharibu wasichana. Tunahitaji vituo vya kuokoa wasichana katika maeneo ya mashinani,”alisema.

Aliwasuta wazazi katika eneo hilo kuhusu ndoa za mapema na watoto kupewa kazi ngumu.

“Wanaoa wanawake wengi ili wabaki nyumbani wakati wao wanahama na mifugo wao kutafuta nyasi na maji.Wanaume wengine huanza kutaka na wasichana wakiwa na miaka tatu,”akisema.

Bw Moroto alisema kuwa viongozi wako msitari wa mbele kupigana na visa hivyo kwa jamii.

Amon Maket, mvulana ambaye alipewa mafunzo alisema kuwa ukeketaji umeathiri wasichana wengi katika eneo hilo.

Msichana Dorcas Chesang alisema kuwa wamenufaika pakubwa na mafunzo hayo.

You can share this post!

Vijana washindwa kumzuia Simba Arati kuhutubia

Waititu aajiri madaktari 40 wapya kuboresha huduma

adminleo