TSC yalipa Sh466m kwa walimu-hewa, yasema inajikaza kuzikomboa
NA CHARLES WASONGA
IMEFICHUKA kuwa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) imelipa Sh466 milioni kama mishahara kwa walimu-hewa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa bungeni mnamo Jumanne na tume hiyo, pesa hizo zililipwa kwa walimu ambao ama ni wafu, waliacha kazi au wamekuwa wakitelekeza kazi, katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.
Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia alikabiliwa na wakati mgumu kuwaelezea wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uhasibu (PAC) jinsi tume hiyo ilivyolipa kiasi hicho kikubwa cha pesa pasina kung’amua kuwa walimu hao hawakuwa kazini.
Dkt Macharia alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Maalum John Mbadi kujibu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu, kuhusu matumizi ya fedha katika TSC katika mwaka huo wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2022.
Hii ndio maana wanachama wa PAC waliamuru uchunguzi wa kina kufanywa katika orodha ya malipo ya mishahara wa tume hiyo kubaini “ukweli halisi kuhusu hasara hiyo.”
“Nadhani ipo haja ya mifumo ya TSC ya ulipaji mishahara ifanyiwe ukaguzi wa kina. Naamini kuna hitilafu kubwa katika TSC. Isiposhughulikiwa inaweza kuzalisha sakata kubwa,” akasema Mbunge wa Soy David Kiplagat.
Bw Mbadi aliunga mkono pendekezo hilo huku akihoji jinsi TSC iliruhusu ulipaji mishahara kwa walimu ambao walikuwa wamekufa kitambo.
“Swali, ambalo linahitaji kujibiwa baada ya ukaguzi huu ni nani alikuwa akipokea pesa hizo Sh466 milioni ilhali waliolengwa na wafu? Huenda pesa hizo ziliingia kwenye mifuko ya watu binafsi katika TSC,” Bw Mbadi akashuku.
Kwenye ripoti yake ya ukaguzi, Bi Gathungu alikuwa ameibua maswali kuhusu malipo ya pesa hizo Sh466.9 milioni, ambazo ni ongezeko la Sh114 au la bajeti ya Sh352.9 milioni katika mwaka huo wa kifedha wa 2021/2022.
Aidha, PAC ilifahamishwa kwamba TSC ilizongwa na hitilafu nyingine za malipo kuhusiana na matumizi ya pesa kupita kiasi, kupunguzwa kwa michango ya TSC kwa Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) na hazina nyingine kama hizo.
Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema masuala yaliyoibuliwa kwenye ripoti hiyo ni mazito zaidi.
“Ni jambo la ajabu kwamba mwalimu ambaye amekuwa akisusia kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja analipwa mishahara ilhali wengine wanalazimishwa kukaa kwa muda mrefu bila malipo. Ukaguzi huu utabaini ukweli kuhusu chimbuko cha sakata hii,” akaeleza.
Akijitetea, Dkt Macharia alisema alisema kuwa suala ya malipo ya ziada ya mishahara lilitokea kutokana na kucheleweshwa kwa kusitishwa kwa malipo ya mishahara baada ya walimu kufa, kutelekeza majukumu, kujiuzulu, kubadili kazi au kusimamishwa kazi.
“Malipo hayo ya zaidi yamekuwa yakiendelea kwa muda miaka kutokana na utendakazi mbaya wa mifumo ya kuripoti masuala kama hayo. Hii ni kwa sababu shughuli hiyo inafanywa kwa njia ya kawaida sio kielektroniki hali ambayo inacheleweshwa kupatika kwa habari kuhusu, kwa mfano, idadi ya walimu waliokufa au wale ambao wameacha kazi na kuajiriwa kwingineko,” Dkt Macharia akawaelezea wanachama wa PAC katika majengo ya bunge, Nairobi.
Hata hivyo, alisema kama njia ya kuzima hitilafu hiyo TSC imebuni sera kuhusu malipo ya ziada ambayo inateleleza wakati huu.
“Aidha, tumeanzisha mfumo wa kuripoti masuala hayo kupitia mitandao ili kuongeza kasi ya shughuli hiyo. Mfumo huo umeunganishwa kati ya makao makuu ya TSC, maafisa wa nyanjani na shule ili kubaini visa vya walimu kufa, kujiuzulu au kutelekeza kazi,” Dkt Macharia akaeleza.
Aliongeza kuwa TSC pia imejuza wakuu wa taasisi mbalimbali za kielimu, makurugenzi wa elimu katika ngazi za kaunti ndogo na kaunti kuhusu suala hilo la malipo ya kupitia kiasi.
Dkt Macharia pia aliwahakikishia wabunge wanachama wa PAC kwamba “TSC inaendelea na mchakato wa kukomboa pesa hizo zilizolipwa kimakosa kwa walimu hewa.”
Kwa mfano, alitoa barua moja ambayo TSC ilimwandikia Alice Sawe ikimtaka kurejesha Sh260,110 ambazo zililipwa kwa mumewe, Sawe Robert Kipleting, kwa miezi minne ilhali alikuwa amekufa.
Katika barua hiyo TSC inatisha kukomboa pesa hizo kwa “kutumia njia za kisheria zilizoko” ikiwa Bi Sawe atafeli kurejesha pesa hizo.
Tume hiyo pia imemwandikia Mercy Awino Yogo ikimjuza kurejesha Sh24,671.30 ambazo ni malipo kupitiliza aliyolipwa kati ya Oktoba 12, 2021, na Oktoba 31, 2021
TSC hiyo pia imeandikia benki na vyama kadha vya akiba na mikopo ikiwemo chama cha kitaifa cha Akiba na Mikopo cha Walimu (Mwalimu National Sacco) kurejesha Sh149,995 za Bernard Kinyua Mathenge ambaye alikufa kuiwezesha kutayarisha malipo yake ya mwisho kwa jamaa zake.