Habari za Kitaifa

Mama, meidi wake wanyakwa kwa kukosa taarifa msingi za mtoto wa siku mbili

February 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA BRIAN OCHARO

WANAWAKE wawili wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na ulanguzi wa watoto baada ya kushindwa kutoa taarifa za msingi kuhusu mahali na tarehe ya kuzaliwa kwa mtoto wa siku mbili.

Bi Margaret Katini Mwasaka na mfanyakazi wake wa nyumbani, Clara Mugandi, walijikuta pabaya baada ya kupatikana wakiwa na mtoto huyo mwenye umri wa siku mbili.

Kwa sasa, wote wawili wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central ambapo wapelelezi kutoka Kitengo cha Kulinda Watoto jijini Mombasa wanatafuta majibu kuhusiana na asili ya mtoto huyo.

Jambo la kushangaza ni kwamba Bi Mwasaka, anayedaiwa kuwa mama wa mtoto huyo, hakuweza kutoa maelezo ya kimsingi kuhusu mtoto huyo, ikiwa ni pamoja na historia yake ya ujauzito, wapi na lini alijifungua.

Tukio hilo liligunduliwa wakati mwanamke huyo alipompeleka mtoto huyo katika Hospitali ya Premier mnamo Februari 15.

Aliandamana na msaidizi wake wa nyumbani. Hata hivyo, hakuweza kutoa taarifa za msingi ambazo mama wa rika lake hapaswi kusahau siku mbili tu baada ya kujifungua.

“Bi Mwasaka hakuweza kueleza ni lini na wapi mtoto huyo alizaliwa na hakuweza kutoa historia ya kabla ya kujifungua,” Inspekta Francis Maina ambaye anachunguza kisa hicho alisema.

Bi Mwasaka na Mugandi walifikishwa katika mahakama ya Shanzu, ambapo wapelelezi waliomba kuwazuia kwa wiki mbili ili kuchunguza kikamilifu suala hilo.

Bw Maina alimweleza Hakimu Mwandamizi Mkuu Yusuf Shikanda kuhusu tuhuma zake kwamba huenda wanawake hao wanahusika katika njama inayohusiana na ulanguzi wa watoto wachanga.

Stakabadhi zozote

Mpelelezi huyo pia alitembelea hospitali hiyo, na kuthibitisha kuwa Bi Mwasaka hakuwa na stakabadhi zozote za ujauzito wa miezi tisa hadi kudaiwa kuzaliwa kwa mtoto mnamo Februari mwaka huu.

“Baada ya uchunguzi wa awali katika hospitali hiyo, nilibaini kuwa Bi Mwasaka alitembelea hospitali ya Premier Oktoba 2, 2023, na uchunguzi ukafanywa ambao ulihitimisha kwamba hakuwa na ushahidi wa ujauzito,” alisema Bw Maina.

Anapanga kutumia siku 14 zijazo kufanya tathmini ya kina ya matibabu ya mtoto huyo ambaye amelazwa hospitalini kwa sasa. Mpelelezi pia analenga kukusanya ushuhuda muhimu kutoka kwa mashahidi na kupata ushahidi wa DNA ili kubaini uzazi wa mtoto huyo.

“Washukiwa wengine ambao tunashuku wanahusika katika njama ya ulanguzi wa watoto bado hawajakamatwa. Uchunguzi unaendelea ili kuwapata na kuwabaini wazazi wa kibaolojia wa mtoto huyo,” alisema.

Afisa huyo alielezea hofu kuwa washukiwa hao, kwa sasa wanafahamu makosa yanayochunguzwa hivyo huenda wakaingilia uchunguzi na mashahidi wakiachiliwa kwa dhamana.

“Bi Mwasaka amekuwa akiwasiliana na wahusika wengine na kwa hivyo, kuna haja ya kuchunguza simu zake,” alisema afisa huyo na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo si wa mwanamke huyo.

Mwanamke huyo, kupitia kwa wakili wake Paul Magolo, alichagua kutozungumzia ikiwa mtoto huyo ni wake au la, badala yake aliamua kukaa kimya kuhusu suala hilo. Washukiwa hao walidai kuwa dhamana ni haki yao ya kikatiba na kwamba Serikali haikutoa sababu zozote za msingi za kuwanyima dhamana.

“Hatuoni sababu ya kuongeza muda wa kuzuiliwa kwetu. Simu zetu ziko mikononi mwa polisi, kwa hivyo hakuna msingi wa kutuzuia zaidi,” walisema kupitia Bw Magolo.

Uchunguzi kufanyika

Wakili huyo alisisitiza kwamba uchunguzi unapaswa kuja kabla ya washukiwa kukamatwa.

“Bi Mugandi alikuwa msaidizi wa Bi Mwasaka nyumbani, hakuna chochote kilichosemwa dhidi yake. Tunaiomba mahakama kuwaachilia kwa dhamana,” alisema.

Hata hivyo, Hakimu Shikanda aliruhusu polisi kuwazuia washukiwa hao akibaini kuwa walikosa kujibu tuhuma zilizowasilishwa na serikali dhidi yao.

Mahakama ilikubali kuwa uchunguzi wa kina ulikuwa muhimu ili kubaini uzazi wa mtoto na ushiriki wa wahojiwa katika mtandao wa uhalifu huo wa ulanguzi wa watoto wachanga.

“Ikiwa simulizi ya Serikali ni jambo la kweli basi ninakubali kwamba kuna uwezekano kuwa tunafanya kesi ya ulanguzi wa watoto. Hilo si suala la kuchukuliwa kirahisi,” alisema hakimu.

Hakimu huyo alikubaliana na mashaka ya serikali kuwa washukiwa wanaweza kuwa sehemu ya mtandao mkubwa unaojihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu, akiangazia hitaji la kuwaweka washukiwa kizuizini wakati wa uchunguzi.