Kamati yabuniwa kuchunguza madai dhidi ya waziri wa Ardhi Taita Taveta
NA LUCY MKANYIKA
BUNGE la Kaunti ya Taita Taveta limeunda kamati maalum ya kuchunguza madai ya ukiukaji wa maadili yanayomkabili Waziri wa Ardhi Elizabeth Mkongo.
Hatua hiyo imefuatia hoja iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi Hope Anisa mnamo Jumanne wiki hii, ambayo ilipitishwa na wawakilishi wengi wa bunge hilo.
Bi Anisa alisema kuwa Bi Mkongo ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kusababisha migogoro mingi ya ardhi katika kaunti hiyo.
Kamati hiyo maalum itaongozwa na Bw Amos Makalo, ambaye ni mwakilishi wa wadi ya Kasigau na vilevile naibu wa kiongozi wa wachache.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Bi Rose Shingira, Bw Anselm Mwadime, Bi Dorcas Mlughu na Bw Isaac Matolo.
Akiongoza hoja ya kuunda kamati hiyo, Naibu Spika Bw Mwadime aliitaka kamati hiyo kufanya uchunguzi kwa usawa na uadilifu na kuzingatia sheria zilizowekwa.
Alisema kuwa bunge hilo bado linaendelea na mchakato wa kumtimua Bi Mkongo ambaye atapewa nafasi ya kujitetea mbele ya kamati hiyo.
Mwakilishi wa Wadi ya Wundanyi Bw Jimmy Mwamidi, aliitaka kamati hiyo kutumia hekima katika uchunguzi wake ili kumpa Bi Mkongo nafasi ya kusikizwa.
“Matokeo yoyote ambayo kamati hiyo itafikia hayapaswi kukiuka kanuni zilizoko zikiwemo kusikizwa kwa pande zote,” alisema Bw Mwamidi.
Kamati hiyo ina siku kumi kuchunguza madai dhidi ya Bi Mkongo na kuwasilisha ripoti yake katika bunge hilo.
Ripoti hiyo itaamua hatma ya Bi Mkongo ambaye anatishiwa kufutwa kazi.
Hata hivyo, Bi Mkongo amekanusha madai hayo na kusema kuwa ni njama ya baadhi ya wawakilishi kumharibia jina na kumzuia kufanya kazi yake.
Wakati huohuo, bunge hilo limeagiza ukaguzi wa vyeti vya maafisa wote wa kaunti ili kuhakikisha kuwa wana vyeti halali na stahiki.
Akiongoza hoja hiyo, Kiongozi wa Wachache Bungeni Genard Mwandau alisema kuwa maafisa wa kaunti wanatoa huduma muhimu zinazogusa maisha na ustawi wa wananchi na kwamba huduma hizo zinapaswa kutolewa na watu waliohitimu.
Bw Mwandau alisema kuwa maafisa ambao wenye vyeti ghushi huisababishia serikali ya kaunti madhara ya kisheria kutokana na kutoa huduma duni.
“Ni haki ya wananchi kupata huduma bora kutoka kwa kaunti yao. Ndiposa zoezi hili ni la muhimu,” alisema Bw Mwandau.
Bunge hilo limeitaka serikali ya kaunti kupitia kaimu katibu wa kaunti Bw Habib Mruttu kukamilisha ukaguzi wa vyeti vya maafisa wake ndani ya siku sitini na kuwasilisha ripoti hiyo bungeni.