Wakulima wa viazi wakadiria hasara baada ya bakteria kuharibu mimea
NA PETER CHANGTOEK
BAADHI ya wakulima wanaokuza viazi katika eneo la Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu, wanalia kwa kupata hasara kubwa baada ya viazi walivyopanda kuanza kuoza katika mashamba yao.
Wanasema kuwa, walizinunua mbegu za viazi kutoka kwa kampuni moja kubwa nchini inayouza mbegu, na wanailaumu kampuni hiyo kwa hasara waliyopata.
Mkulima Julius Ragor, mkuzaji viazi katika eneo la Sugoi, anasema kuwa asilimia 80 ya viazi alivyopanda katika shamba lake vimeharibika kwa kuoza.
Anafichua kuwa, alikuwa amenunua viazi magunia 22 ya kilo 50 kila moja, aina ya Markis kwa bei ya Sh4,200 na kuvipanda katika shamba lake.
“Nilinunua Desemba 13, 2023, na kupanda baada ya siku nne. Nilitumia Sh103,400 – Sh92,400 kwa mbegu na Sh500 kusafirisha kila gunia,” akasema Bw Ragor, aliyetumia Sh11,000 kusafirisha mbegu zote hadi shambani mwake.
Mkulima huyo anasema kwamba, viazi vingi havikuota, na alipojaribu kuchimbua ili ajue sababu iliyofanya kutoota, akapigwa na butwaa kugundua kuwa vilikuwa vimeoza udongoni.
Anaongeza kuwa, viazi vilivyokuwa vimefanikiwa kuota vilianza kunyauka na kuangamia kwa sababu ya ugonjwa wa kuoza, uliosababishwa na bakteria.
Ragor anadokeza kuwa, amepoteza kima cha takribani Sh200,000 kwa jumla, ikiwemo ghrama aliyotumia katika shughuli ya kuandaa shamba, mbegu na nguvukazi.
Anafichua kuwa, wakulima wengine pamoja naye, waliandikia baruapepe taasisi ya Kephis, na ikawatuma maafisa wake shambani, waliochukua sampuli za viazi vilivyoharibika.
Hata hivyo, anasema kuwa, si mara yake ya kwanza kuzinunua mbegu kutoka kwa kampuni hiyo. Alizinunua mbegu kutoka kwa kampuni hiyo mwaka 2022, na kuzipanda katika shamba lake, ambapo alivuna tani 13.
Anaongeza kwamba, alikuwa amezipanda mbegu hizo kwa kutumia mbinu ya kunyunyizia maji, na maji hayakuathiri mimea hiyo.
Ken Lagat, ni mkulima mwengine katika eneo hilo. Anasema kuwa alikuwa amezipanda mbegu za viazi Desemba 2023, katika shamba ekari mbili.
“Nilinunua magunia 22 kwa Sh4,000 kwa kila gunia, na nikapanda siku nne baadaye. Vilianza kuoza baada ya wiki mbili,” asema, akiongeza kuwa, vilioza kabla havijaota na pia baada ya kumea.
“Tuliwasiliana na kampuni hiyo pamoja na Kephis baada ya siku 21, kupitia kwa baruapepe, lakini Kephis ikaja kuchukua sampuli kutoka kwa shamba,” afichua Lagat.
Anasema kuwa, amepoteza takribani Sh400,000 ambazo alikuwa akitarajia kutoka kwa mazao ambayo angepata, endapo mimea yake isingeharibika shambani.
Alikuwa akitarajia kupata tani 40 za viazi baada ya mavuno, jambao ambali halijawezekana kwa sababu ya ugonjwa huo.
Hosea Rugut, mkulima mwengine kutoka eneo la Sugoi, anasema kuwa, alikuwa amezinunua mbegu za viazi magunia 72, kila moja likiwa na kilo 50.
“Nilinunua kutoka kwa kampuni ya Agrico PSA. Mbegu hizo zilianza kuoza baada ya kupanda. Shamba lote limeathirika. Ningezalisha tani 20 kwa kila ekari,” afichua mkulima huyo, aliyekuwa amezipanda mbegu kwa shamba ekari sita.
Mkulima mwengine, ambaye hakutaka kutajwa, alisema kuwa, shamba lake limeathiriwa na bakteria zilizokuwa kwa mbegu.
“Nilinunua magunia 20 kwa Sh3,500 kwa kila gunia,” akasema mkulima huyo, akiongeza kuwa alikuwa amezinunua za saizi ndogo.
Ripoti ambayo iliandaliwa na Kephis baada ya kupeleka sampuli za viazi kutoka kwa shamba la Rugut, inadhihirisha dhahiri shahiri kuwa, sampuli hizo zilikuwa na bakteria aina ya Pectobacterium na Dickeya spp. Sampuli hizo zilikuwa zimechukuliwa kutoka shambani na Kennedy Muteti, afisa wa Kephis anayehudumu mjini Eldoret.
Hata hivyo, mmojawapo wa wakurugenzi wa kampuni ya Agrico PSA, anasema kuwa Hosea Rugut peke yake ndiye aliyezinunua mbegu kutoka kwa kampuni hiyo, na kuongeza kwamba, wakulima hao wengine tuliowahoji walinunua kutoka kwa mkulima huyo.
“Tunashirikiana na Kephis ili kubaini kilichosababisha kuoza kwa viazi hivyo,” akasema mkurugenzi huyo, wa kampuni hiyo iliyoko jijini Nakuru.