Habari za Kitaifa

KWAHERI STAA: Kelvin Kiptum akimbia mbio zake za mwisho duniani

February 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

WINGU la simanzi limetanda katika boma la marehemu mwanariadha Kelvin Kiptum eneo la Chepsamo safari yake ya mwisho iking’oa nanga.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya mbio za Marathon atazikwa leo Ijumaa baada ya kukamilika kwa ibada kabla ya mazishi inayoendelea katika uwanja wa Chepkorio Show.

Msafara wa jeneza lake likisindikizwa na waombolezaji umepitia katika kituo cha biashara cha Chepkorio ambapo mamia ya wenyeji walisimama kando kando ya barabara kuutazama msafara huo.

Baadhi yao walitiririkwa machozi huku wakipiga picha kwa kutumia simu zao za mkononi.

Shughuli za biashara zilinoga katika soko la Chepkorio ambapo wageni waliohudhuria mazishi hayo ndio walikuwa wateja wakuu.

Pundu tu baada ya mwili kufikishwa uwanjani, maduka karibu yote yalifungwa na wauzaji wakajiunga na wageni kwenye ibada kabla ya mazishi.

“Kwa kipindi cha wiki moja, biashara imeimarika katika soko hili hasa biashara ya chakula ambapo wageni wanaokuja kuomboleza wamekuwa wamekuwa wakinunua bidhaa,” amesema Marion Chepkoi ambaye ni mzaliwa wa Chepkorio.

Katika uwanja wa Chepkorio kulikuwa na shughuli si haba haswa baada ya mwili kuasili mwendo wa saa tatu na dakika 13.

Rais William Ruto, maafisa wakuu katika serikali ya Kenya Kwanza na wageni wengine wa kimataifa, wamewasili kwa staili tofauti.

Wanahabari wa humu nchini na wa kimataifa hawajaachwa nyuma kwani nao pia wanaendelea kupeperusha sherehe hiyo kupitia kwa vyombo tafauti.

Waombolezi wamepewa takribani dakika 10 kuutazama mwili kabla ya Kanisa la Angilikana (ACK) kuanza rasmi ibada husika.