Mtunzaji wa bwawa azuiliwa kufuatia kifo cha mwanafunzi shuleni
Hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani Geoffrey Onsarigo aliwaruhusu makachero kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kumhoji Geoffrey Juma Opala kubaini kilichojiri kabla ya mwanafunzi huyo kuzama na kuaga dunia mnamo Februari 20, 2024.
Bw Onsarigo alisema polisi wanahitaji muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi wa kina kwa lengo la kubaini iwapo mtunzaji huyo wa bwawa la shule alizembea kazini.
“Hii mahakama imesikiliza ombi la polisi kwamba mshukiwa huyu azuiliwe siku saba na kufikia uamuzi kwamba azma yao iko na mashiko kisheria na inaambatana na Katiba,” alisema hakimu.
Pia alisema mahakama inafahamu kwamba suala hilo liko na umuhimu mkubwa ikitiliwa maanani wazazi wa mtoto aliyeaga dunia wako na machungu pamoja na washika dau wengine.
Mahakama iliombwa imnyime mshukiwa huyo dhamana kwa ajili ya usalama wake.
“Wazazi wa shule ya Visa Oshwal walighadhabishwa na kitendo cha Bw Opala kutomzuia mtoto huyo kujitosa majini na kufa. Naomba mahakama imnyime mshukiwa huyu dhamana,” alisema Konstebo Clare Wafula.
Mahakama ilielezwa mshukiwa huyo alimwona mvulana huyo wa Gredi ya Kwanza akielekea katika bwawa la kuogelea.
Mwili wa mwanafunzi huyo ulionekana Februari 20,2024.
Bw Opala alikuwa kazini siku hiyo.
“Bw Opala anachunguzwa kwa kosa la kuzembea kazini kinyume cha sheria nambari 128,” alisema Bi Wafula.
“Mshukiwa huyu alinaswa na camera za CCTV akiwa kazini wakati marehemu alipompita kwenye lango na kuelekea upande wa bwawa hilo,” hakimu alifahamishwa.
Mahakama ilielezwa mshukiwa huyo atavuruga uchunguzi kwa kuwashawishi mashahidi wengine kutoandikisha taarifa za ushahidi.
Wengi wa mashahidi ni wafanyakazi wenza.
Akitoa uamuzi, hakimu alisema suala hilo la mtoto kufia shuleni linahitaji kuchangamkiwa kwa upesi.
Alisema mshukiwa alikuwa amejificha na anahitaji kuhojiwa kwa makini.
Hakimu aliamuru mshukiwa azuiliwe hadi Machi 4, 2024, atakaporudishwa kortini kwa maagizo zaidi.