Mvulana auawa kwa kupigwa risasi na majangili Pokot Magharibi
NA OSCAR KAKAI
TAHARUKI inaendelea kutanda kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Turkana baada ya mvulana wa umri wa miaka 12 kuuawa Ijumaa kwa kupigwa risasi eneo la Takaiywa na majangili wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani ya Turkana.
Kijana aliyeuawa alikuwa mgonjwa na alikumbana na mauti akiwa kwa pikipiki na babake na mamake akipelekwa kupata matibabu katika zahanati ya Turkwel ambapo walivamiwa njiani huku kijana huyo akiuawa na wazazi wake wakiponea kifo chupuchupu na kupata majeraha madogo baada ya kutoroka.
Kijiji cha Takaiywa kimekuwa eneo la makabiliano kati ya majangili na wakazi, hali inayoibua hofu na taharuki kuu.
Mwezi Januari, askari wa akiba aliuawa kwenye kijiji hicho akishika doria karibu na shule ya Lonyangelem.
Haya yanajiri baada ya serikali kutuma askari wa akiba 205 kwenye maeneo hatari ya kaunti ya Pokot Magharibi.
Akiongea na Taifa Leo Jumamosi asubuhi, naibu kamishina katika eneo la Pokot Kaskazini James Ajuang alithibitisha tukio hilo akisema kuwa lengo la uvamizi huo halijulikani.
“Majangili hao waliua kijana huyo na kutorokea kwenye msitu,” alisema Bw Ajuang.
Bw Ajuang alisema kuwa maafisa wa usalama wametumwa katika eneo hilo kutuliza hali ya taharuki.
“Hatutakubali mtu yeyote kuhusika na visa vya wizi wa mifugo,” akaonya.
Chifu wa Ombolion Joseph Korkimul alisema kuwa washukiwa hao walitokea eneo la Namakat, Kaunti ya Turkana.
“Kijiji hiki kimekuwa hatari sasa na tunahitaji kuwa na mbinu za kisasa kutatua shida hii. Tunahitaji askari wengi wa akiba. Hatuwezi kupoteza watu kila siku. Mwezi jana nipoteza askari wa akiba ambaye ni mtu wa familia yangu na bado ninaomboleza,”alisema Bw Korkimul.
Alisema kuwa wakazi kwa sasa wanaishi kwenye hofu akisema kuwa kwa miezi kadhaa majangili kutoka kaunti ya Turkana wamekuwa wakivamia vijiji na kuiba mifugo.
“Wakazi kwa sasa hawalali kwenye nyumba zao sababu ya kuhofia mashambulizi mapya,” alisema.
Alisema kuwa hivi maajuzi askari wa akiba aliuawa eneo la Takaiywa na majangili wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani ya Turkana.
Bw Korkimul aliitaka serikali kujenga vituo maafisa wa kupambana na wizi wa mifugo katika maeneo ya Takaywa na Ombolion ili kukomesha ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama.
“Chanjo cha uvamizi huo hakijabainka na ninaomba serikali kutuma maafisa wengi wa usalama katika eneo hili ili kuimarisha usalama,” alisema.
Viongozi wa eneo hilo walilaani mashambulio hayo na kuitaka serikali kuchunguza kuhusu chanzo cha mashambulio ya mara kwa mara.
Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing alisema kuwa huenda serikali isiafiki malengo yake ya kunyamazisha milio ya risasi eneo la Bonde la Kerio ikiwa haitatumia viongozi wa eneo hilo kutatua shida hiyo.
“Serikali inatumia mbinu mbaya. Huwezi kutishia viongozi kila wakati. Hapana. Serikali inachochea viongozi kuhusika kwenye vita. Amani huja kwa mazungumzo. Ukitishia viongozi wanakuwa mashujaa kwa jamii zao,” alisema Bw Pkosing.
Seneta wa Kaunti ya Pokot Magharibi Julius Murgor alitoa wito kwa mshirikishi wa eneo la Bonde la Ufa Abdi Hassan kuingilia kati ili kutuliza hali.
“Waziri wa Usalama Kithure Kindiki anafaa kuacha kushika viongozi bali afanye mazungumzo,” alisema kasisi Murgor.
Kasisi Murgor aidha alizitaka jamii zote mbili kukumbatia amani.
“Sisi ni majirani na tunafaa kujifunza kuishi pamoja. Hakuna yeyote atakayenufaika na wizi wa mifugo na ujangili. Eneo hili linahitaji miradi ya maendeleo kama unyunyuziaji maji mashamba, shule na makanisa na serikali inafaa kulipa wahubiri waeneze injili katika eneo hili,” alisema.
Alisema kuwa operesheni ya usalama ambayo inafanywa na serikal haijawahi kufaulu.
“Rais mstaafu hayati Mwai Kibaki alitumia mazungumzo na kulikuwa na amani. Watu wetu waliachwa nyuma kimaendeleo. Ni uchungu mama kupoteza mzee na mtoto ambaye alimbeba miezi tisa tumboni,” aliongeza.