Habari za Kitaifa

Wakenya ni miongoni mwa 25 waliofariki katika ajali Tanzania

February 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LABAAN SHABAAN

WAKENYA ni miongoni mwa watu 25 waliofariki katika ajali Arusha, nchini Tanzania.

Ajali hiyo ilitokea saa kumi na moja jioni mnamo Februari 24, 2024 katika Barabara Kuu ya Arusha – Namanga ikihusisha magari manne.

Watu wengine 21 walijeruhiwa.

Tukio hilo lilithibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Afisi ya Rais Samia Suluhu, Zuhura Yunus ambaye alituma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa waliofariki.

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mkoa wa Arusha Justine Masejo, maafa hayo yanahusisha raia kutoka mataifa saba; Kenya, Togo, Madagascar, Burkina Faso, Afrika Kusini, Nigeria na Amerika.

Taarifa ya Rais haijabainisha idadi ya Wakenya waliofariki.

Hata hivyo, ilitaja walioaga dunia walikuwa wanawake 10, wanaume 14 na mtoto mmoja wa kike.

Bw Masejo alieleza kwamba ajali hiyo ilihusisha gari la mizigo ya Kampuni ya Kay Construction ya Kenya.

Lori hilo lililokuwa linatoka Namanga kuelekea Arusha liligonga magari matatu ya abiria.

Moja ya magari hayo ni matatu na jingine ni gari la kibinafsi.

Gari la shule ya New Vision Tanzania lilikuwa linabeba raia wa kigeni waliokuwa wanafanya kazi ya kujitolea kwenye shule hiyo.

Polisi wanaendeleza msako kusaka dereva wa lori ambaye yuko mafichoni.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa lori hilo lilikumbwa na mushkil wa breki kabla ya kupoteza mwelekeo na kugonga magari mengine.