Waziri Mvurya ahimiza Wanakwale kuchangamkia elimu kufukuza umaskini
NA KNA
WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Baharini na Ubaharia, Bw Salim Mvurya, amewataka wakazi wa Kwale kuichangamkia elimu na kuitambua kuwa ndiyo njia bora ya kukuza maarifa na kukomesha umaskini na magonjwa.
Bw Mvurya alisema hayo katika eneobunge la Kinango katika hafla ya uzinduzi wa vyumba viwili vya madarasa na maabara na kukabidhi basi jipya la shule katika Shule ya Upili ya Salim Mvurya.
Alieleza kuwa, serikali ya kitaifa itaendelea kusaidia maendeleo ya miundomsingi ya shule za upili za Kwale ili kuwapa nafasi wanafunzi wengi wanaovuka kutoka kiwango cha elimu ya msingi hadi sekondari.
Waziri Mvurya alikuwa ameandamana na Gavana wa Kwale Fatuma Achani na Mbunge wa Kinango Gonzi Rai ambapo pia alitoa wito wa ushirikiano kutoka kwa wadau wengine wa elimu kusaidia kupunguza idadi ya watoto wasioenda shuleni katika kaunti hiyo.
Aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni kulingana na sera ya mpito ya asilimia 100 kutoka ngazi ya elimu ya msingi hadi ya upili inayosimamiwa na serikali ya kitaifa.
Kwa upande wake, Bi Achani alisema serikali ya kaunti ililenga kuimarisha sekta ya elimu katika eneo hilo ili kuwa kielelezo ambacho kaunti zingine zingeiga.
Bi Achani alizidi kusema kuwa, kaunti imeongeza mgao wa kila mwaka wa mpango wa ‘Elimu Ni Sasa’ kutoka Sh400 milioni hadi Sh500 milioni ili kufaidi wanafunzi zaidi wa vyuo vikuu na shule za upili.