Tanzia: Dunia yamwomboleza mwanamuziki Peter Morgan
NA WANDERI KAMAU
DUNIA inaendelea kumwomboleza mwanamuziki-kiongozi wa kundi la Morgan Heritage kutoka Jamaica, Peter Morgan.
Kundi hilo linafahamika kote duniani kutokana na utunzi wake wa kipekee wa nyimbo za miondoko ya Reggae.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na kundi hilo, mwanamuziki huyo, maarufu kama “Peeter”, alifariki Jumapili, Februari 25, 2024.
Kundi hilo, hata hivyo, halikueleza sababu ya kifo cha msanii huyo.
“Ni kwa mapenzi tunatangaza kwamba mume wetu mpendwa, baba, mwana na ndugu na mwanamuziki-kiongozi wa kundi la Morgan Heritage, Peter Anthony Morgan ametuacha leo (Jumapili),” likasema.
“Familia yetu inawashukuru kwa mapenzi yenu na uungwaji mkono, na tunawaomba kundelea kutuombea tunapoyapitia haya. Pia, tunawaomba kutupa muda wa kuomboleza na tunapondelea kuhimiliki hali hii.”
Peter Morgan ni miongoni mwa watoto zaidi ya 20 wa mwanamuziki Denroy Morgan kutoka Jamaica.
Alizaliwa mnamo Julai 11, 1977 katika eneo la Brooklyn, jijini New York, Amerika.
Kundi hilo lilibuniwa 1994 na ndugu watano wa familia ya Morgan.
Tangu kubuniwa kwake, kundi hilo liliibukia kuwa kipenzi kwa Wakenya wengi.
Limefanya makumi ya shoo nchini, kiasi kwamba 2015 wanachama wake walitangaza nia ya kununua shamba na kuhamia Kenya.
Kundi lilitoa tangazo hilo baada ya maswali kuzuka, lilipokaa sana nchini, licha ya kumaliza kutumbuiza kwenye shoo lilizotarajiwa kuwatumbuiza mashabiki wake.
Wanachama walisema walikuwa na mipango ya kununua mashamba ya kulima na nyumba jijini Nairobi.
Kwa miaka kadhaa, wamekuwa wakionekana katika sehemu tofauti nchini. Walikuwa hata wakitoa maoni yao kuhusu masuala yaliyokuwa yakiendelea nchini.
Kwa mfano, wakati Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alizindua usajili wa Huduma Namba 2019, kundi hilo lilikuwa miongoni mwa wanamuziki waliojitokeza wazi kurai Wakenya kujisajili kwa idadi kubwa.
Miongoni mwa Wakenya walioeleza kusikitishwa na kifo cha mwanamuziki huyo ni Refigah, aliyekuwa mmiliki wa studio ya Grandpa Records.
Refigah amehusika kwenye shughuli za kuandaa shoo kadhaa za wanamuziki maarufu wa Raggae kutoka Jamaica, kwa mfano Eric Donaldson.
“Ni pigo kubwa kwa mashabiki wa Reggae nchini na duniani kote,” akasema.
Baadhi ya nyimbo maarufu za kundi hilo ni ‘She’s Still Loving Me’, ‘I’m Coming Home’, ’Tell Me How Come’ kati ya nyingine nyingi.