Elimu, kilimo kutengewa fedha zaidi kwenye bajeti ijayo
NA TITUS OMINDE
SEKTA ya elimu inatazamiwa kupata sehemu kubwa ya mgao wa bajeti ya kitaifa ya Sh4.2 trilioni kwa mwaka wa kifedha wa 2024/2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa Ndindi Nyoro, ambaye pia ni mbunge wa Kiharu, amefichua mbali na idara ya elimu vile vile sekta ya kilimo itanufaika pakubwa.
Akihutubu katika eneobunge la Kapseret wakati wa kuzindua hazina ya elimu ya Sh6.6 milioni kutoka NG-CDF kwa mwaliko wa mbunge wa eneo hilo Oscar Sudi, Bw Nyoro alisema sekta ya elimu ina jukumu muhimu katika kuunda mustakabali wa nchi na hiyo ndio maana inastahili mgao zaidi.
Kulingana na Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) ya 2024 katika Bunge la Kitaifa, idara za Elimu na Kilimo zitapata asilimia kubwa ya bajeti nzima.
“Katika Taarifa ya Sera ya Bajeti ya Mwaka wa Kifedha 2024/2025, sekta za elimu na kilimo zimetengewa bajeti kubwa. Elimu ina jukumu muhimu katika kuunda mustakabali wa nchi ndio maana tumeweka bajeti kubwa kwa sekta hiyo,” akafichua Bw Nyoro.
Bw Nyoro alisema pia serikali ya Kenya Kwanza inataka kuvutia wakulima zaidi katika kilimo ili kuhakikisha kwamba wanakumbatia kilimo-biashara pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula.
Huku akiwapongeza wakulima kwa jukumu wanalotekeleza katika uchumi wa nchi, Bw Nyoro alisema bajeti kubwa iliyotengwa kwa ajili ya kilimo itaingia kwenye ununuzi wa pembejeo za kilimo kama vile mbolea ili kuhakikisha wakulima wanazalisha chakula cha kutosha.
“Tunataka kilimo kiwe biashara yenye faida kwa kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea ya ruzuku kama kichocheo kinachovutia wakulima zaidi,” alisema mbunge huyo wa Kiharu.
Bw Nyoro alisema sekta zote kuu za kilimo zitawekwa kunufaika na mbolea ya serikali ya bei nafuu.
Miongoni mwa wakulima ambao wanatazamiwa kufaidika na mbolea ya ruzuku katika mwaka ujao wa kifedha ni pamoja na wakulima wa nafaka, kahawa, majanichai, pamba, na miwa miongoni mwa wakulima wa mazao mengine.