Wazazi sasa watoa watoto shule za kibinafsi kwa kulemewa na uchumi
MAMIA ya wazazi wamehamisha watoto wao kutoka shule za kibinafsi na kuwapeleka shule za umma kutokana na hali ngumu ya maisha.
Udadisi uliofanywa na Taifa Leo umeonyesha idadi kubwa zaidi ya wanafunzi waliohamishwa Januari kutoka shule za kibinafsi licha ya changamoto tele zinazokumba taasisi za umma kama vile ukosefu wa miundomsingi na walimu wa kutosha.
Familia zimelazimika kubadilisha matumizi yao ya kifedha huku gharama ya elimu ikiibuka kuwa suala nyeti.
Wazazi waliokuwa wakimudu kwa urahisi elimu katika shule za kibinafsi sasa wamejipata waking’ang’ana kutokana na misukosuko kazini, mishahara kupunguzwa, mfumko wa bei kupanda na shinikizo nyinginezo za kifedha.
Wasimamizi wa shule za kibinafsi waliozungumza na wanahabari wamekiri vilevile kuwa wazazi wanadaiwa mamilioni ya pesa na taasisi hizo na kwamba wengi wao wameingia kwenye miafaka ya kulipa.
Japo wamekanusha kuwa wanafunzi wanahama kwa wingi kutoka shule zao, takwimu zilizokusanywa kutoka shule za umma zinaashiria vinginevyo.
Katika muda wa miezi miwili pekee, Shule ya Msingi ya Bungoma DEB imepokea zaidi ya wanafunzi 300 wapya waliohama shule nyinginezo.
Miongoni mwao, 200 wanatoka shule za kibinafsi almaarufu academies.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Bungoma DEM, Tobias Khisa, alifichua kwamba ongezeko hilo katika idadi ya wanafunzi wapya limeongeza mzigo kwa miundomsingi na rasilimali za shule hiyo.
Shule hiyo iliyokuwa na wanafunzi 4,391, sasa inakabiliwa na misongamano madarasani huku walimu wakifanyishwa kazi zaidi ili kufidia ongezeko hilo la ghafla.
“Kwa sasa tuna walimu 103 kutoka TSC ambapo idadi ya wanafunzi ikilinganishwa na walimu imepiku kiwango kinachohitajika hivyo kusababisha shinikizo.
“Katika shule za msingi hasa, idadi hiyo ni 1:63, huku hali ikizorota zaidi katika madarasa ya chini ambapo idadi ni 1:70. Hali hii imechangiwa na kuongezeka kwa wanafunzi wanaohamia shule za umma kutoka shule za kibinafsi,” alisema Bw Khisa.
Kulingana na Bw Khisa, kubadilisha shule kuna madhara kwa wanafunzi.
Idadi ya wanafunzi wanaohamia shule za kibinafsi kutoka shule za umma imeongezeka kwa asilimia tano katika shule moja iliyopo jijini Nairobi huku wazazi wakihusisha uamuzi wao na nyakati ngumu za maisha.
Mwenyekiti wa Muungano wa Shule za Kibinafsi, Charles Ochome alisema shule zina namna mbalimbali za kukabiliana na wazazi wanaoshindwa kulipa karo kwa wakati.
“Hiyo inatarajiwa. Hali ya uchumi si shwari vile lakini hatuwashinikizi wazazi kulipa kiasi chote mara moja.”
Inategemea jinsi usimamizi wa shule unavyohusiana na wazazi,” alisema Bw Ochome.
Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu alieleza Taifa Leo kuwa Wizara yake inafahamu kuhusu uhamisho huo na athari zake kwa miundomsingi na ubora wa elimu katika shule za kibinafsi.