Siasa

Raila amepenya serikalini?

February 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka kuhusu ikiwa kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, hatimaye ameingia serikalini, baada ya kuanza kutangamana na viongozi wakuu wa serikali ya Kenya Kwanza, akiwemo Rais William Ruto.

Bw Odinga pia amekuwa akitangamana na mawaziri.

Mnamo Jumatatu, iliibuka kwamba Bw Odinga aliandamana na Rais William Ruto kuenda nchini Uganda, kumrai Rais Yoweri Museveni kumuunga Bw Odinga mkono kwenye azma yake ya kuwania ueneyekiti katika Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Februari mwaka ujao.

Hayo yanajiri licha ya tofauti kubwa za kisiasa ambazo zimekuwepo baina ya Bw Odinga na Rais Ruto hapo awali, hasa kuhusu maandamano ambayo Bw Odinga alikuwa akiongoza dhidi ya serikali kuhusiana na kupanda kwa gharama ya maisha.

Baada ya picha kuhusu ziara ya Rais Ruto na Bw Odinga nchini Uganda, kiongozi huyo alitoa taarifa akimshukuru Rais Ruto kwa kuanza harakati za kumfanyia kampeni kuwania nafasi hiyo.

“Ninamshukuru Rais Ruto kwa kuandamana nami nchini Uganda kunifanyia kampeni kuhusu nia yangu ya kuwania nafasi ya uenyekiti katika AUC,” akasema Bw Odinga.

Duru zimeiambia Taifa Leo kuwa tayari, serikali imetenga fedha za kufadhili safari za maafisa wa ngazi za juu serikalini kusafiri katika mataifa tofauti barani Afrika, kuwarai viongozi wake kumpigia kura Bw Odinga kuchukua nafasi hiyo.

Hayo pia yanajiri huku baadhi ya mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza wakianza kufika katika afisi za Bw Odinga kumweleza kuhusu hali ya utendakazi katika wizara zao.

Mnamo Jumanne, Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, alifika katika afisi za Capitol Hill, zake Bw Odinga, ambapo alimwelezea hatua ambazo amechukua katika kutimiza usawa wa kijinsia katika idara tofauti za kiserikali nchini.

Wawili hao baadaye walifanya mazungumzo na hata kupigwa picha.

Kando na hayo, imeibuka kuwa kuna uwezekano baadhi ya washirika wa Bw Odinga watakeuliwa kwenye nyadhifa kuu serikalini.

Kutokana na hayo, baadhi ya wadadisi wanasema kuwa kuna uwezekano kuna makubaliano ambayo Rais Ruto na Bw Odinga waliafikiana walipofanya kikao cha faragha jijini Mombasa mwaka uliopita, chini ya uwepo wa rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

“Naamini kwamba haya ni matokeo ya mazungumzo ya faragha baina ya Rais Ruto na Bw Odinga. Ikiwa haya ndio matokeo, basi huenda tukashuhudia mabadiliko serikalini katika siku zijazo. Lazima tuelewe kwamba Bw Odinga ni mwanasiasa mwerevu, ambaye amekuwa akitumia ushawishi wake kuhakikisha anafaidika kutoka kwa serikali inayochukua uongozi,” asema Bw Martin Andati, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.