Siasa

Simba Arati sasa amtetea Dkt Monda

February 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

GAVANA wa Kisii Simba Arati amewarai madiwani kutathmini upya hoja inayolenga kumng’atua afisini naibu wake Dkt Robert Monda.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini, amesema angependa madiwani hao wampe muda asuluhishe tofauti zilizoko baina yake na Dkt Monda bila kumjadili bungeni kwa faida ya ustawi wa maendeleo ya gatuzi hilo.

Gavana Arati aliyasema hayo mnamo Jumatano baada ya kukutana na viongozi wa makanisa na madhehebu mengine katika eneo la ATC.

“Ninatoa wito kwa MCAs. Najua mmechukua msimamo mkali kuhusu suala la naibu wangu. Linagusa afisi yangu na kwa hivyo ninaomba mtafakari upya msimamao wenu. Licha ya kuwa mmetenga Alhamisi iwe siku ya kujadili hoja hiyo, mtupeni nafasi tuongee nje ya bunge,” gavana Arati akasema.

Gavana wa Kisii Simba Arati. PICHA | MAKTABA

Kauli ya kiongozi huyo iliungwa mkono na maaskofu na wachungaji waliokuwa kwenye kikao hicho.

Sasa inakisiwa kuwa huenda hoja iliyofikishwa katika bunge la kaunti hiyo kuhusu Dkt Monda ikaondolewa.

Diwani wa Ichuni Wycliffe Siocha ndiye aliyewasilisha hoja ya kutaka mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache ang’atuliwe afisini.

Bw Siocha anatoka ukoo mmoja na Dkt Monda, ukoo wa Abanyaribari, na hatua yake ya kutaka kiongozi kutoka ukoo wake ‘amwage unga’ ilifasiriwa na wengi kama ‘usaliti’.

Siasa za viti vya kaunti katika jamii ya Abagusii zimejengeka pakubwa katika kigezo cha ukoo na kila ukoo hujaribu kutetea mtu wao anapoandamwa kisiasa kinyume na alivyofanya Bw Siocha.

Kufuatia kwenda kinyume na mapenzi ya watu wa ukoo wake, Bw Siocha amekuwa akipokea kashfa za kila aina kutoka kwa watu wa Nyaribari kwa kuleta hoja hiyo.

Ili kutetea hoja yake, diwani Siocha alimtuhumu Dkt Monda kwa ufisadi na matumizi mabaya ya afisi yake.

Madiwani wanaolenga kumng’atua mamlakani Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda watoa sababu tatu za kumtaka mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache atimuliwe. Madai hayo ni kwamba Dkt Monda alipokea hongo ya Sh800,000 kutoka kwa mkazi mmoja aliyekuwa akitafuta kazi, matumizi mabaya ya afisi yake, na kujaribu kuhujumu uteuzi wa Meneja wa Mauzo wa Kampuni ya Maji ya Gusii, GWASCO. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Gavana Arati hajawa na uhusiano mzuri na naibu wake tangu Novemba mwaka jana wakati Dkt Monda aliwakaribisha nyumbani kwake wakosoaji  wa kisiasa wa bosi wake.

wakosoaji hao ni mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na Japheth Nyakundi wa Kitutu Chache Kaskazini.

Wengine ni Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi na baadhi ya madiwani (MCAs) ambao mnamo Novemba 25, 2023, walikutana na Dkt Monda katika boma lake lililoko kijijini Rigena, eneobunge la Nyaribari Chache. Mkutano huo ulifanyika usiku.

Japo viongozi hao waliwaambia wanahabari kuwa mkutano wao ulikuwa wa kutathmini jinsi ya kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo, ilionekana wazi kwamba viongozi hao walikuwa wakipanga njama kuhusu namna ya kumtenga Gavana Arati dhidi ya viongozi wengine wa kaunti hiyo.

Mkutano huo kwa Dkt Monda ulijiri muda mfupi tu baada ya wanasiasa hao kuhudhuria hafla ya misa katika Kanisa Katoliki la Nyabururu ambapo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alikuwa mgeni wa heshima

[email protected]