Habari za Kitaifa

Wakenya sasa wanachukua mikopo kununua chakula nyumbani

February 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PATRICK ALUSHULA na NINA SHABAN

WAKENYA sasa wanachukua mikopo midogo midogo ya kununua chakula na kutimiza mahitaji mengine ya kimsingi wakati huu ambapo gharama ya juu ya maisha inaendelea kupanda.

Idadi ya Wakenya ambao wamelemewa kulipa mikopo yao nayo inaendelea kupanda kwa kishindo huku kiasi cha pesa wanazodaiwa sasa kikifikia Sh700 bilioni.

Mwenyekiti wa Muungano wa Benki za Kenya John Gachora alisema idadi ya Wakenya ambao wanaendea mikopo kufadhili ujenzi au kupanua biashara zao imepungua sana.

Badala yake, Wakenya wanachukua mikopo midogo midogo kugharimia mahitaji madogo madogo kama chakula.

Kupanda kwa gharama ya maisha, kiwango cha juu cha riba, makato ya ushuru na mengine yaliyokumbatiwa na serikali yamesababisha Wakenya kutokuwa na pesa zinazohitajika kwa matumuzi yao ya kila siku.

“Ukweli ni kuwa katika mazingira kama haya, Wakenya wamelemewa kujimudu kuchukua na kulipia mikopo. Wachache sana wanakopa pesa za kuwekeza kwenye miradi na wengi wanakopa tu hela za kujikimu,” akasema Bw Gachora ambaye pia ni Meneja Mkurugenzi wa NCBA.

Waajiri wengi nao wamelazimika kupuuza Sheria ya Uajiri ya 2007 ambayo inahitaji makato kwenye mshahara wa mfanyakazi yasizidi theluthi mbili ya mshahara wao.

Hii ni kwa sababu serikali imeongeza ada ambazo wafanyakazi wanatozwa kwenye mshahara wao ikiwemo ushuru wa nyumba.

Benki zimeanza kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda Wakenya wakalemewa kulipa hata mikopo hiyo midogo ambayo wanaichukua baada ya kushindwa kulipa ile kutoka kwa kampuni za kutoa pesa kwa njia ya kidijitali.

Takwimu za benki zinaonyesha kuwa idadi ya Wakenya ambao walilemewa kulipa madeni ilipanda hadi asilimia 15.3 mnamo Oktoba, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kwa muda wa miaka 16.

Kiwango hicho kilipungua hadi asilimia 14.8 mnamo Disemba kulingana na Takwimu za Benki Kuu ya Kenya (CBK).

“Hili ni suala ambalo linafaa kutushughulisha sote kwa sababu mikopo haifai kutumika kugharimia mahitaji. Hii ina maana kuwa mishahara yao haitoshi kukidhi mahitaji yao ya kimsingi,

“Ukiwaona watu wakichukua mikopo basi hiyo ina maana kuwa hata theluthi ambayo wanastahili kusalia nayo imeingiliwa. Huwa tunawashauri wafanyakazi waangalie malipo yao kabla ya kuchukua mikopo ya miradi mbalimbali na sasa wengi hawawezi kulipa vyema mikopo yao.

Gharama ya maisha imepanda nchini huku pia mshahara wa chini kabisa kwa mfanyakazi nao haujapandishwa. Wafanyakazi wanaopokea mshahara wamekuwa wakikatwa Sh2160 kwa Hazina ya NSSF ambao ulikuwa Sh200.

Pia malipo yao yamechimbwa kutokana na makato ya asilimia 1.5 ambayo yamekuwa yakielezwa katika Ushuru wa Nyumba.

Makato yataongezeka zaidi kuanzia Julai wakati ambapo asilimia 2.75 ya mshahara utakuwa ukielekezwa kwa Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).

Kwa jumla, asilimia 21 ya mshahara wa Wakenya wanaolipwa zaidi ya Sh50,000 itaishia kwenye makato.