Shahidi katika kesi ya mauaji adai Jumwa alimlima makonde
SHAHIDI katika kesi kuhusu mauaji ya mfuasi wa Chama cha ODM, Jola Ngumbao, amesimulia madai ya jinsi Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa alivyomshambulia kwa mangumi.
Bw Michael Otieno aliambia mahakama ya Mombasa kuwa walikuwa katika makazi ya Reuben Katana mnamo Oktoba 15, 2019, ambapo chama kilikuwa kikitoa mafunzo kwa maajenti wake kabla ya uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda wakati Bi Jumwa alipovamia boma hilo mwendo wa saa kumi na moja jioni.
“Gari lilitokea ghafla. Nilimwona Geoffrey Okuto akishuka kwenye gari na kufuatiwa na Bi Jumwa na wanawake wengine,” shahidi huyo alimweleza Jaji Anne Ongi’njo.
Bw Okuto alikuwa msaidizi wa Bi Jumwa wakati huo. Ameshtakiwa kwa mauaji ya Bw Ngumbao.
Alikuwa ameshtakiwa pamoja na Bi Jumwa lakini Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ilimuondela mbunge huyo wa zamani wa Malindi shtaka hilo.
Upande wa mashtaka uliambia mahakama ushahidi ulipitiwa upya na kubaini kuwa Bi Jumwa hakuhusika katika mauaji ya Bw Ngumbao.
Bw Otieno alidai kuwa, Bi Jumwa alielekea moja kwa moja hadi kwenye hema ambapo maajenti wa uchaguzi na maafisa wengine wa chama hicho walikuwa wakikutana baada ya kushuka kutoka kwa gari lake.
Alisema Mbunge wa Magarini Michael Kingi na madiwani kadha walikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwepo katika hema hilo.
Polisi pia walikuwepo kwenye boma hilo. Bw Otieno alisema maafisa wa usalama walikuwa wamesimama takriban mita 70 kutoka mahali ambapo mkutano huo ulikuwa ukifanyika.
Kulingana na shahidi huyo, walinzi wa Bi Jumwa walijaribu kumshikilia asifike kwenye hema hiyo lakini aliingia kwa fujo na kusababisha mapigano.
“Alirusha ngumi kwa yeyote aliyekuwa mbele yake akisisitiza kwamba mkutano huo hautafanyika,” alisema shahidi huyo ambaye alikuwa akiongozwa na kiongozi wa mashtaka, Bernard Ngiri.
Shahidi huyo alidai kuwa kila mtu pale, akiwemo Bw Kingi, walimsihi mbunge huyo wa zamani asivamie mkutano huo, lakini hakusikia lolote.
“Hata tulimuuliza kwa nini anaingilia mkutano wetu wakati walifanya mkutano wao bila kusumbuliwa,” shahidi huyo alisema.
Bw Otieno alidai kuwa huku viongozi wakimsihi Bi Jumwa asivuruge mkutano huo, mbunge huyo wa zamani alimshambulia Bi Maureen Arawa kwa makonde.
Bi Maureen alikuwa pamoja na Bw Otieno. Bi Jumwa anawafahamu wote wawili kwani wamewahi kuwa pamoja wakati mbunge huyo a zamani alikuwa mwanachama wa Chungwa.
“Nilipomuuliza Bi Jumwa kwa nini alikuwa akimshambulia Bi Arawa, alinigeukia na kunishambulia akidai kuwa tulikuwa katika eneobunge lake, si la Bw Odinga. Alinirushia ngumi usoni na kifuani,” aliambia mahakama.
Bw Otieno alisema mshiriki katika mkutano huo alimrushia kiti mlinzi wa Bi Jumwa. Washiriki wengine walirusha vumbi kwa timu ya Bi Jumwa.
“Maafisa hao walianza kufyatua risasi hewani. Bi Jumwa alinipiga jicho la kulia na kifuani. Nilikimbia kwenda kujificha kwenye nyumba iliyokuwa karibu na eneo lile. Mtu aliyekuwa karibu nami alipigwa risasi na kufa,” alisema.
Bw Otieno alisema baadaye aligundua kuwa mtu aliyekuwa karibu naye ambaye alijeruhiwa kwa risasi hiyo ni Bw Ngumbao.
Shahidi huyo aliendelea kusema kuwa huku hali hiyo ikiendelea, Bw Okuto alirejea kwenye gari na kujihami kwa bastola.
“Bw Okuto alikuwa ameshikilia bastola kwenye mkono wake wa kulia ingawa sikumwona akifyatua risasi. Maafisa waliokuwa karibu walifyatua risasi hewani kutawanya umati,” alifafanua shahidi huyo alipoulizwa na wakili wa mshukiwa Bw Paul Magolo kama aliona Bw Okuto akimpiga risasi mwendazake.
Shahidi huyo alisema alikwenda katika wadi ya Ganda Oktoba 17 kufuatilia uchaguzi huo. Alirekodi taarifa yake na polisi siku iliyofuata.