Jamvi La Siasa

Gachagua @59: Mbele iko sawa?

February 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua mnamo Februari 28, 2024, aliadhimisha siku ya kuzaliwa ambapo alifikisha umri wa miaka 59.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema siku hiyo kwa Bw Gachagua ilikuwa na hisia mseto, ikiwa ni mkondo mgumu lakini muhimu.

“Huyu ni sawa na mchezaji wa akiba katika mchezo wa Ikulu. Mkubwa wake alikuwa Naibu Rais mwaka wa 2022 na leo hii ni Rais. Huo ndio umuhimu wa wadhifa wa Bw Gachagua kwa sasa,” asema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Ngugi Njoroge.

Lakini ndipo afanikiwe kupaa zaidi katika hali za kawaida, Bw Gachagua anahitajika kumenyana na nyangumi wakali katika bahari hiyo.

“Katika hali ya kawaida, Bw Gachagua anaweza akawania urais mwaka wa 2027 au wa 2032. Yeye tayari amekiri kwamba mwaka wa 2027 atamuunga Rais Ruto kusaka awamu ya pili,” asema Prof Njoroge.

Lakini ili akubalike, Bw Gachagua itabidi asake mbinu za haraka za kuibuka mshindi katika changamoto zilizo mbele yake.

“Anafaa kwanza atafute mbinu ya haraka ya kuzima ukaidi katika ngome yake kuu ya Mlima Kenya. Ukaidi huo unamkosesha fursa adimu ya kukubalika na wote kama msemaji wao,” asema aliyekuwa Waziri Msaidizi katika wizara za Spoti na Elimu Zack Kinuthia.

Suala la pili ni kukubalika kwa vita vyake dhidi ya pombe ya mauti Mlimani.

“Hivyo vita si rahisi na vimejaribiwa awali na wengine akiwemo Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mwaka wa 2015 ambaye karibu vimumalize kisiasa. Bw Gachagua amerithi vita hivyo na si rahisi kwa mwanasiasa wa haiba yake,” asema Bw Kinuthia.

Hata hivyo, Bw Gachagua ametoa kauli kwamba “ikiwa nitapoteza umaarufu wangu kupitia vita dhidi ya pombe ya mauti, na iwe hivyo”.

 “Lakini sitakaa kimya huku wafanyabiashara wa pombe ya mauti wakiendelea kuangamiza vizazi na kututwika umaskini,” akasema Bw Gachagua.

Aidha, alitangaza kwamba walevi na watengenezaji wa pombe si watu wa kutegemewa katika kuidhinisha kufaulu kwa mwanasiasa.

Suala jingine ni kukubalika kwake nchini kama kiongozi wa nje ya Mlima Kenya.

“Shida ya Bw Gachagua ni kuwa mara nyingi huegemea Mlima Kenya na kusahau ni kiongozi wa nchi nzima,” adai Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wa Orange Democratic Movement (ODM).

Bw Sifuna anasema kwamba matamshi ya Bw Gachagua kuhusu nchi kuwa ya wanahisa yalimpotezea alama kwa kiwango Fulani miongoni mwa Wakenya wengi.

Naibu Rais pia ana ulazima wa kujinyanyua katika harakati zake za kuhakikisha sekta za kilimo na biashara zinamkumbatia kama mtetezi wa kweli.

Hizo, sekta ni za maana sana katika siasa.

“Aliahidi kuimarisha mapato kwa kuvunja makateli lakini wakulima wengi wanahisi hajafanikiwa ipasavyo. Ufanisi unaweza ukampa guu mbele katika ari yake,” asema mwenyekiti wa muungano wa wakulima wadogowadogo Stephen Kimani.

Bw Gachagua tayari amekiri kwamba mitandao anayopambana nayo katika sekta ya kilimo ni mingi na kwamba makateli hao wana nguvu ajabu.

Lakini ameomba tu subira akisema kabla ya 2027 mambo yatakuwa yameimarika na atakuwa ameangamiza mitandao hiyo.

Bw Gachagua aidha anahitaji uungwaji mkono na mabwanyenye wa hapa nchini na pia aunde mitandao ya washirika katika mataifa ya kigeni ili kupiga kuweka hai ndoto yake.

“Kwa sasa Bw Gachagua hajatanua mbawa ipasavyo. Inafaa aunde mtandao mpana,” asema aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni.

Bw Kioni anasema kwamba Bw Gachagua ana wakati mgumu wa kutetea umuhimu wake katika siasa za Mlima Kenya, kitaifa, Afrika Mashariki, Barani na pia kote ulimwenguni.

Aidha, Bw Gachagua pia anafaa ajue namna ya kutangamana na vijana damu moto wasije wakamsumbua.

Katika uchaguzi wa 2027 Bw Gachagua atakuwa akielekea umri wa miaka 64 huku uchaguzi wa 2032 ukimpata akielekea umri wa miaka 70 majaliwa.

Kwa upande mwingine, vijana kama mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye amekuwa akivizia mamlaka ya Bw Gachagua–japo alikanusha–watakuwa chini ya umri wa miaka 50. Wadadisi hao wanahisi wanasiasa damu moto wanaweza kumtatiza katika jumuiya ya wapigakura ambao kwa kiwango kikuu watakuwa ni vijana.

[email protected]