Kocha mpya wa Gor amsifia winga aliyezima Lobi Stars ya Nigeria
NA CECIL ODONGO
KOCHA mpya wa Gor Mahia Hassan Oktay amemlimbikizia sifa kedekede winga wa klabu hiyo Samuel Onyango baada ya mwanadimba huyo kuyafunga mabao mawili muhimu kwenye ushindi wa 3-1 waliosajili dhidi ya Lobi Stars ya Nigeria Jumapili Disemba 16.
Mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika iligaragazwa kwenye uga wa MISC Kasarani jijini Nairobi.
Mchezaji huyo wa zamani wa mabingwa wa KPL mwaka wa 2011 alitia msumari moto kwenye kidonda cha wageni hao baada ya mvamizi wa K’Ogalo raia wa Rwanda Jacques Tuyisenge kufunga bao safi kwa kujipinda mapema kipindi cha cha mchuano huo.
Ingawa mabao hayo mawili ndiyo yalikuwa ya kwanza kwa Onyango kwenye dira ya Bara, kiwango cha juu cha mchezo aliyodhihirisha sasa kitamkosesha usingizi winga mwenza George ‘Blackberry’ Odhiambo ambaye huenda akaanza kusugua benchi uchezaji wake usipoimarika.
Akizungumza baada ya mtanange huo, Oktay alimsifu winga huyo kwa uchezaji mzuri.
“Samuel ni mchezaji mzuri anayejivunia ukwasi wa talanta na wakati mwingine unafaa kuwapa wachezaji nafasi ya kuridhisha uwezo wao kikosini na uwatilie shime kwamba wanaweza kung’aa. Huwezi kuwapuuza mchezaji kila wakati ila unafaa kumkuza,” akasema Oktay, semi zilizoonekana kumlenga Odhiambo ambaye amekuwa akihimili nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Mkondo wa pili wa mtange huo utasakatwa Ijumaa Disemba 21 nchini Nigeria. Lobi Stars watahitaji kuifunga Gor Mahia mabao mawili.