Gachagua aahidi kuendelea kurudisha sekta ya chai kwa laini
NA CHARLES WASONGA
NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa wadau mbalimbali katika sekta ya majanichai kuondoa kesi walizowasilisha kortini alizodai zinahujumu utekelezaji wa mageuzi katika sekta hiyo.
Akiongea Alhamisi wakati wa kutolewa rasmi kwa ripoti ya utendakazi wa sekta hiyo katika mwaka wa 2023, Bw Gachagua alisema kesi hizo zinawazuia wakulima kufaidi kutokana na jasho lao.
Naibu Rais alisema ni makosa kwa baadhi ya wadau kuwasilisha kesi kortini ili kuzuia wakulima kupata faida katika sekta hiyo tajiri.
“Kesi zilizoko mahakamani zinayumbisha mageuzi katika sekta hii ndogo na muhimu. Natoa wito kwa wadau kuondoa kesi hizo ikiwa wanataka sekta ya majani inawiri. Waondoe kesi hizi ili tuweze kutekeleza mageuzi faafu kwa manufaa ya wakulima wadogowadogo wa majanichai,” Bw Gachagua akasema.
Alitoa mfano wa wakurugenzi wa Shirika la Kustawisha Chai Nchini (KTDA) ambao wamewasilisha kesi dhidi ya bodi ya shirika hilo, ilhali wametangaza azma ya kuwania nyadhifa mbalimbali za ukurugenzi wa bodi za viwanda vya majanichai.
“Unawezaje kuishtaki KTDA kuhusiana na masuala ambayo hayahusiani na masilahi ya wakulima kisha unageuka na kutaka kuwania kiti cha kuwa mkurugenzi wa kiwanda kilichoko chini ya usimamizi wa KTDA au katika KTDA yenyewe?” akauliza.
Alisema wanachama wa kampuni zilizoko chini ya usimamizi wa KTDA, hawawezi kuwania nyadhifa katika shirika hilo.
“Inasikitisha kuwa watu hawa wanaoongozwa na uchu wa mamlaka wamewapeleka wakulima kortini na mawakili wao wanalipwa kutumia pesa zilizofaa kuwafikia wakulima. Hii sio sawa na ni kielelezo cha utovu wa adabu na maadili. Unawezaje kudai kuwa unawajali wakulima ilhali unatumia pesa zao kufadhili kesi dhidi yao mahakamani? Kesi zinaendeleza masilahi yenu finyu wala sio ya wakulima wengine,” Bw Gachagua akaeleza alipozindua ripoti kuhusu utendakazi wa sekta ya majanichai katika makao makuu ya Bodi ya Chai Kenya (TBK) jijini Nairobi.
Bw Gachagua alisema kuwa serikali itasimamia na kutoa ulinzi wakati wa uchaguzi ujao wa wakurugenzi wa KTDA na bodi za usimamizi za viwanda vya majanichai vinavyosimamiwa na shirika hili.
“Wakati huu ambapo viwanda vinajiandaa kwa chaguzi, tunatoa wito kwa wakulima kuzingatia maadili kwamba uongozi mzuri utaendeleza na kulinda mageuzi ambayo tunatekeleza katika sekta ndogo ya majanichai,” akaeleza.
Wakati huo huo, Bw Gachagua aliwataka maafisa wa utawala kushirikiana na maafisa wa wa TBK kuwakamata wale wanaoshiriki katika uchuuzi wa majanichai.
“Tumetoa maagizo kwa maafisa wa utawala wa serikali kuu kuunga mkono TBK kuhakikisha wale wanaoendesha uchuuzi wa majanichai wanakamatwa na kushtakiwa kortini. Hii ni kwa sababu hatutaki kuruhusu wahalifu kuharibu sekta ya majanichai,” akaeleza.
Kwa mujibu wa ripoti iliyozinduliwa Alhamisi, Kenya iliuza kilo milioni 522.92 za majanichai mnamo mwaka 2023 kutoka kilo 450.33 milioni zilizouzwa mnamo 2022.
Hii inawakilisha ongezeko la kima cha asilimia 16 (sawa na kilo 72.58 milioni).
Mapato kutokana na mauzo ya majanichai pia yaliongezeka hadi Sh180.57 bilioni kutoka Sh138.09 bilioni mnamo 2022.
Ongezeko hilo la uzalishaji wa majanichai 2023 lilichangiwa na mvua nzuri iliyoshuhudiwa nchini kati ya Aprili na Desemba 2023 na utekelezaji wa mpango wa serikali wa usambazaji mbolea ya bei nafuu.
Kabla ya serikali ya Rais William Ruto kuingia mamlakani mnamo Septemba 13, 2022, bei ya mbolea ilkuwa Sh6,000 kwa gunia moja la kilo 50.
Wakati huu, bidhaa hiyo inauzwa kwa Sh2,500 kwa gunia moja la kilo 50.
Bw Gachagua pia alisema afisi yake inaendeleza mpango wa kupanua soko la majanichai katika mataifa ya ng’ambo.
“Hii ndio maana hivi karibuni nitasafiri hadi Iran ili kujadiliana na maafisa wake kuhusu jinsi ambavyo tutarejesha soko la majanichai yetu katika nchi hiyo. Izingatiwe kuwa zamani Iran ilikuwa mnunuzi mkubwa wa majanichai yetu,” akaeleza.
Bw Gachagua alisema kuwa majanichai ya Kenya ni bora zaidi duniani. Lakini, kulingana na Naibu huyo wa Rais, shida kuu imekuwa upatikanaji wa majanichai ya Kenya katika masoko hayo ya ng’ambo.
Bw Gachagua vile vile alisema kurejeshwa kwa TBK kumerejesha hali nzuri katika sekta ya majanichai ambayo imezongwa na changamoto nyingi.
“Tangu sekta ya majanichai ilipowekwa chini ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) sekta hii imepitia wakati mgumu na ilielekea kuangamia. Kwa hivyo, sasa ambapo TBK imerejeshwa kuisimamia, wakulima wetu wameanza kuchuma matunda kupitia kuongezeka kwa faida,” Bw Gachagua akasema.
Alieleza kuwa katika mwaka huu, wakulima wa majanichai wanatarajiwa kuuza majanichai yao kwa kutoka Sh59, katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023 kwa kilo hadi Sh90 kwa kilo katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027.
Bw Gachagua alisema baada ya kufufuliwa kwa TBK kama asasi ya kusimamia sekta hiyo, “tunatafakari pia kuunda upya Bodi ya Kahawa ya Kenya (CBK).”
“Hii ni kwa sababu sekta hizi mbili ni muhimu zaidi kwa uchumi wetu. Zinafaa kujisimamia zenyewe,” akasema.
Bw Gachagua pia alisema serikali kuu, serikali za kaunti na asasi mbalimbali katika sekta ya chai zitashirikiana kuendeleza uzalishaji wa chai aina ya “orthodox tea”.
“Aina hii ya chai inahitajila kwa wingi zaidi katika masoko ya kimataifa,” akaeleza.