Habari za Kitaifa

Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda afungishwa virago

February 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

NAIBU Gavana wa Kisii Dkt Robert Monda ametimuliwa afisini na madiwani wa gatuzi hilo baada ya hoja iliyowasilishwa bungeni dhidi yake kupita.

Madiwani 53 walipiga kura Dkt Monda aende nyumbani ilhali wengine 15 walipiga kumwokoa.

Diwani mmoja hakupiga kura.

Kulingana na jinsi kura hiyo ilivyoenda, madiwani hao waliafikia kigezo cha thuluthi mbili kinachohitajika kisheria kumtuma Dkt Monda nyumbani.

Bunge hilo lina jumla ya madiwani 70. MCAs 45 wanawakilisha maeneo yao ilhali wengine ni maalum.

Dkt Monda alituhumiwa na madiwani hao kwamba alichukua hongo ya Sh800,000 ili asaidie mkazi mmoja wa Kisii apate kazi katika Kampuni ya Maji na Majitaka ya GWASCO.  Lakini kazi hiyo haikupatikana na hilo lilipelekea aliyepaswa kuajiriwa kunung’unika.

Mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache pia alisemekana kutumia afisi yake vibaya kwa kujaribu kumhonga Meneja Mkurugenzi wa GWASCO ili mtu wake apate kazi hiyo.

Pia Dkt Monda alidaiwa kumnyanyasa nduguye waliyekuwa na mzozo naye kuhusu ni nani mmiliki wa miti iliyo katika shamba la baba yao.

Akijibu shtuma hizo bungeni Alhamisi, Februari 29, 2024, Dkt Monda alitoa maelezo kuhusu madai hayo ifuatavyo:

Kuhusu ikiwa alipokea hongo ya Sh800,000 kutoka kwa mkazi mmoja wa Kisii ili amsaidie kupata kazi katika Kampuni ya Maji na Majitaka ya GWASCO, Dkt Monda alisema pesa hizo zilikuwa za deni alilokuwa amekopesha babake mlalamishi.

Kuhusu ikiwa alimtumia Meneja Mkurugenzi wa GWASCO hongo ya Sh100,000 ili meneja huyo amsaidie mtu wake apate kazi ya Meneja wa Mauzo wa kampuni hiyo ya GWASCO, Naibu Gavana alisema alituma pesa hizo ‘kimakosa’.

“Pesa hizo zilikuwa zimwendee afisa mmoja wa kaunti kwa kazi aliyonifanyia ya kusafirisha bidhaa za ujenzi nyumbani kwangu. Nilifikiri pesa hizo zilimwendea aliyefaa kuzipokea kumbe haikuwa hivyo. Nilibaini hilo wakati Meneja aliniuliza ni za nini keshoye,” akajitetea Dkt Monda.

Shtaka la tatu lilikuwa ikiwa aliwatumia vibaya maafisa wa kutekeleza amri za kaunti kwa kuwafanya vibarua katika shamba lake. Lakini akijitetea, Dkt Monda alisema hafanyi ukulima wowote wala ufugaji wowote wa ng’ombe katika kipande cha ardhi alichorithi kutoka kwa babake. Hata hivyo Dkt Monda alikiri kuhusika katika kutiwa mbaroni kwa nduguye waliyekuwa wakizozania miti.

Katika juhudi za kujaribu kumwokoa Naibu wake, Gavana Simba Arati alijaribu kuwarai madiwani kuisitisha hoja ya “kumwaga unga” Dkt Monda lakini madiwani hao walimkaidi na kuendeleza na hoja hiyo.

Dkt Monda alikuwa bungeni wakati wa kura hiyo pamoja na mkewe, Bi Joyce Monda.

Katika kujibu mashtaka dhidi yake, Naibu Gavana alisaidiana na mawakili wake Katwa Kigen na Wilkins Ochoki.

Gavana Arati hajawa na uhusiano mzuri na naibu wake tangu Novemba mwaka jana wakati Dkt Monda aliwakaribisha nyumbani kwake wakosoaji wa kisiasa wa bosi wake.

Wakosoaji hao ni mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na mwenzake wa Kitutu Chache Kaskazini Japheth Nyakundi.

Wengine ni Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi na baadhi ya madiwani (MCAs) ambao mnamo Novemba 25, 2023, walikutana na Dkt Monda katika boma lake lililoko kijijini Rigena, eneobunge la Nyaribari Chache.

Mkutano huo ulifanyika usiku.

Japo viongozi hao waliwaambia wanahabari kuwa mkutano wao ulikuwa wa kutathmini jinsi ya kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo, ilionekana wazi kwamba viongozi hao walikuwa wakipanga njama kuhusu namna ya kumtenga Gavana Arati dhidi ya viongozi wengine wa kaunti hiyo.

Kufuatia kutimuliwa kwa Dkt Monda, sasa Spika wa Bunge la Kisii Dkt Philip Nyanumba atamfahamisha mwenzake wa Seneti kuhusu uamuzi uliofanywa na madiwani hao.

Ikiwa maseneta wataridhishwa na uamuzi wa MCAs hao, basi Dkt Monda atapoteza wadhfa wake na ikiwa seneti itamwokoa, atarejea kuhudumu katika kiti chake.

[email protected]