Wakazi Bonde la Ufa wauliza Rais atatimiza ahadi lini
NA ERIC MATARA
AKIFANYA kampeni zake za uchaguzi wa 2022, Rais William Ruto aliahidi kutekeleza miradi muhimu katika eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa katika mwaka wake wa kwanza mamlakani.
Hata hivyo, zaidi ya mwaka mmoja baadaye, ahadi hizi hazijatekelezwa, na kusababisha wasiwasi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Miradi ya mabilioni ya pesa, ambayo baadhi ilikuwa imekwama, wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, ni pamoja na barabara, mabwawa makubwa, maeneo ya viwanda, nyumba za bei nafuu na viwanja vya michezo vya kisasa.
Mwaka mmoja akiwa madarakani, ahadi bado zimesalia hivyo; ahadi. Wakazi wa eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa sasa wana wasiwasi kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa.
Mjini Nakuru kwa mfano, Rais Ruto aliahidi kufufua ujenzi wa bwawa la Itare lililokwama huko Kuresoi. Bwawa hilo linakadiriwa kugharimu Sh38 milioni.
Lakini, zaidi ya mwaka mmoja, tangu aingie madarakani, ujenzi wa bwawa hilo kubwa bado haujaanza tena.
Wakazi wameelezea kusikitishwa na mradi huo kuchelewa kutekelezwa.
“Bwawa la Itare lilikusudiwa kutatua tatizo la uhaba wa maji mjini Nakuru na kaunti jirani. Bado tunasubiri ujenzi wa bwawa hilo kufufuliwa kama alivyoahidi rais.Wakati huo huo, tunaendelea kuteseka na tumegeukia kuchimba visima vya maji kushughulikia masuala ya uhaba wa maji,” mkazi wa Kuresoi Kusini, Bw Joseph Towett, aliambia Taifa Leo.
Bi Beatrice Korir, mkazi wa Kuresoi Kaskazini alisema; “Mradi huu umecheleweshwa kwa muda mrefu. Kukamilika kwa mradi huu kutamaliza kabisa uhaba wa maji Kuresoi, Jiji la Nakuru na kaunti jirani. Ninamuomba Rais William Ruto kufufua ujenzi wa bwawa hilo haraka iwezekanavyo,” akasema Bi Korir.
Gavana Susan Kihika amekuwa na matumaini kuwa ujenzi uliokwama wa mradi huo utafufuliwa.
“Nitawasiliana na Serikali ya Kitaifa ili kuhakikisha kuwa tunapata mwanakandarasi wa kukamilisha bwawa la Itare na pia kufanya mazungumzo na Kaunti ya Baringo kwa usambazaji wa maji kutoka bwawa la Chemususu hadi kaunti ndogo za Rongai na Subukia,” alisema Bi Kihika.
Kulingana na Bi Kihika, ujenzi wa bwawa hilo utatoa suluhu ya kudumu kwa changamoto za maji eneo hilo pamoja na kutoa maji kwa kilimo.
Rais Ruto alikuwa ameapa kufufua ujenzi katika mwaka wake wa kwanza ofisini, ili kumaliza changamoto za kudumu za maji katika eneo la South Rift. Kulingana na Dkt Ruto, mradi huo uliokwama 2018, ulihujumiwa na siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.