Habari za Kaunti

Maji: Pwani kuzidi kuteseka serikali ikisitisha mradi

February 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LUCY MKANYIKA

WAKAZI wa ukanda wa Pwani watalazimika kuendelea kuvumilia uhaba wa maji eneo hilo, baada ya serikali kusitisha mpango wa kutekeleza mradi mkubwa ambao ungeleta afueni.

Waziri wa Maji na Usafi, Bw Zachariah Njeru, alisema serikali inatafuta mbinu mpya ya kutekeleza mradi wa awamu ya pili ya bomba la Mzima, almaarufu kama Mzima 2, uliokadiriwa kugharimu Sh35 bilioni.

Mnamo Jumatano, waziri huyo aliambia Seneti kuwa mradi huo ambao ulikusudiwa kusambaza maji kwa Kaunti za Taita Taveta, Kwale, Mombasa na Kilifi, ulisitishwa kwa sababu ulikuwa ghali mno na haukuvutia wawekezaji na hivyo serikali ikakosa fedha za kuutekeleza.

Mradi huo ulitarajiwa kuongeza kiwango cha maji kinachosambazwa kwa kaunti hizo kila siku ili kutatua uhaba ambao umekuwepo kwa miaka mingi, na unazidi kutatiza wakazi kwa sababu ya ongezeko la watu.

“Baada ya kuufanyia tathmini, mradi ulisitishwa. Tunafanya kila tuwezalo kuona vile utaanza upya kwa njia ambayo hatutakuwa na shida kwa sababu ulikuwa ghali na haukuvutia wawekezaji. Tunataka kuanza mchakato mzima tena na tunafanya tathmini nyingine,” Bw Njeru alisema.

Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Seneta wa Taita Taveta, Bw Jones Mwaruma, ambaye alitaka kujua sababu za kucheleweshwa kwa mradi huo kwa miaka mingi.

Seneta huyo amekuwa akielezea wasiwasi wake kuhusu kuchelewa kwa mradi huo ambao ulitarajiwa kuanza Septemba mwaka uliopita.

Akirejelea taarifa iliyotolewa na mtangulizi wake, Bi Alice Wahome, mnamo mwezi Aprili mwaka jana, seneta huyo alimtaka Bw Njeru, kueleza sababu za kuchelewa na kutaka ufafanuzi kuhusu tarehe inayotarajiwa ya kuanza kwa mradi huo.

Waziri huyo wa zamani alikuwa ameliambia bunge kuwa mradi huo ungefanywa kupitia mfumo wa ushirikiano wa serikali na wawekezaji binafsi (PPP).

“Mwaka jana aliyekuwa waziri wa maji alikuwa hapa na alisema kuwa mradi huu ungeanza mwezi Septemba. Nataka kujua kwa nini mradi haujaanza na utaanza lini,” Seneta huyo alisema.

Mradi huo ulikuwa ahadi ya kampeni kwa wakazi na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta na aliyekuwa naibu wake wa wakati huo William Ruto wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2017. Serikali iliahidi kuanzisha mradi huo mwaka 2018.

Mradi huo ulibuniwa kusaidia bomba lililopo la Mzima, ambalo lilijengwa mnamo 1966 na linasambaza maji kwa wakazi wa Taita Taveta, Mombasa na sehemu zingine za Kwale na Kilifi. Bomba hilo limekuwa likipasuka mara kwa mara.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba la kilomita 220 kutoka chemichemi ya Mzima inayopatikana katika mbuga ya kitaifa ya Tsavo Magharibi hadi kaunti za Pwani, pamoja na mitambo ya kusafisha maji, matangi ya kuyahifadhi na mitandao ya usambazaji.

Wakati wa kampeni zake kwa uchaguzi wa urais wa 2022, Dkt Ruto aliahidi kutekeleza mradi huo mara tu atakapochukua hatamu za uongozi.

Wakati wa ziara yake mwezi Julai mwaka jana, Rais alisema mradi huo ulikuwa karibu kutekelezwa na aliahidi kuzindua ujenzi wake kabla ya mwezi Desemba mwaka jana.

Alifichua kuwa aliamuru kurekebisha bajeti ya mradi huo baada ya kugundua kuwa ilikuwa imeongezwa pakubwa.

Rais Ruto aliwahakikishia wakazi kuwa serikali ilijitolea kupata suluhisho inayofaa kwa mradi huo na kuhakikisha kuwa itatatua shida ya uhaba wa maji katika eneo la Pwani.

Kusitishwa kwa mradi huo kumezima matumaini ya wakazi wengi wa Taita Taveta ambao sasa wanashutumu serikali kwa kupuuza mahitaji yao ya maji na kukaidi ahadi zake.