Wakulima wa ndizi Taita Taveta watafutiwa soko kimataifa
Na WINNIE ATIENO
ZAIDI ya wakulima 500 wadogo wa ndizi wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti ya Taita Taveta kuwatafutia soko la kimataifa.
Wakulima hao wa ndizi za kienyeji wataanza kuuza mazao yao katika nchi ya Denmark baada ya serikali yao ya kaunti kutia saini na soko hilo.
Kupitia mradi wa MESPT, serikali hiyo itaanza kusafirisha ndizi tani 700.
Wakulima hao watasafirisha mazao yao kwa kampuni ya Orana inayojihusisha na matunda.
MESPT pia itawezesha wakulima hao kupanda migomba 126,000.
“Soko hili la kimataifa litawawezesha wakulima wetu kupata mapato bora zaidi. Kaunti yetu itakuwa ya kwanza kusafirisha zao hilo la kienyeji ughaibuni,” alisema Waziri wa Kilimo Bw Erickson Kyongo.
Alisema kiwanda cha kutengeneza ndizi kitafufuliwa kupitia mkataba kati ya serikali hiyo na kampuni ya Matunda ya Orana.
“Kiwanda hicho ambacho kilikwama kitafufuliwa na ujenzi wake kumaliziwa hii itafungua ajira kwa zaidi ya wakazi 800. Vile vile kiwanda hicho kitatumika kutengeneza sodo kutokana na mgomba wa ndizi,” aliongeza waziri huyo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya matunda ya Orana Bw Niels Osterberg alisema waklulima hao pia watapewa mafunzo maalum ya ukulima wa ndizi ili waongeze mapato yao.
Aliwasihi wakulima kuongeza ukulima wa ndizi kutokana na soko hilo la kimataifa.
Alisema wataendelea kusajili wkaulima zaidi wa ndizi ili wapate bidhaa nyingi za kuuza huko ng’ambo.
Kulingana na takwimu za wizara ya kilimo, kaunti hiyo inazaidi ya wakulima 6000. Ndizi hizo zimepandwa kwenye ekari 4104 huku wakulima wakivuna tani 65, 280.
Taita Taveta ni kaunti ya pili bora katika ukulima wa ndizi baada ya Kisii kulingana na takwimu za wizara ya kilimo, hata hivyo ukosefu wa soko imekuwa changamoto kubwa kwa wakulima.