Siasa

Sina domodomo isipokuwa kazi tu – Wamatangi

March 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LAWRENCE ONGARO

GAVANA wa Kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi amewasuta mahasimu wake wa kisiasa akisema hana wakati wa kupoteza.

Akihutubu katika ukumbi wa Thika alipofanya kikao na wakazi wa Thika ili kutathmini ni kazi ipi amefanya tangu ashike mamlaka, alisema lengo lake kuu kwa wakati huu ni kuona ya kwamba anatimiza ahadi alizotoa kwa wenyeji na wakazi wa Kiambu kwa kuchapa kazi.

Aliwashauri mahasimu wake kutuliza boli akisema baada ya miaka mitano, kila mwanasiasa atarejea kwa mwananchi na ripoti yake ya matokeo ili waamue ni kiongozi yupi alitimiza ahadi yake ipasavyo.

“Mimi kawaida yangu huwa hamnisikii nikiropokwa maneno ovyo kuwajibu viongozi hao kwa sababu mwenendo wangu hauniruhusu kufanya hivyo,” alijitetea gavana Wamatangi.

Alisema katika kaunti yote ya Kiambu tayari amejenga madarasa 104 ya chekechea, maendeleo aliyosema wazazi wengi wanafurahia.

Wakazi wa Thika wafuatilia hotuba ya Gavana wa Kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi alipowahutubia akiwa katika ukumbi wa Thika mnamo Machi 1, 2024. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Aliahidi kujenga masoko ya kisasa katika kila Kaunti ndogo iliyoko Kiambu ili kila mchuuzi apate nafasi yake ya kuendesha biashara.

Alizuru kijiji cha mabanda cha Kiandutu kilichoko mjini Thika ambacho kwa sasa kinaitwa Diaspora.

Alisema kufikia Juni 2024 kijiji hicho kitakuwa na maji safi na barabara za vichochoro zitakarabatiwa kuwa za lami, hatua itakayopanua wigo wa upatikanaji wa nafasi za ajira kwa vijana.

Alisema siasa za mwaka 2027 ziko mbali mno na kwa hivyo, aliye na nia ya kurejea tena uongozini ni sharti awajibike vilivyo kwa wananchi.

“Hakuna haja ya kujipiga kifua ukisema ni lazima gavana aondolewe mamlakani kwani wananchi ndio mabosi wangu,” akafoka.

Aliahidi kuhakikisha kiwango cha chini cha basari kinakuwa ni kiasi cha Sh5,000 bila ubaguzi wa kutoa fedha hizo.

Alisema afisi yake iko wazi kwa mwananchi yeyote aliye na shida ya kutatuliwa kwani yuko afisini kwa ajili ya wananchi.