Makala

Kang’ethe kuendelea kuzuiliwa hadi Machi 13

March 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MHANDISI wa ndege nchini Marekani Kevin Kang’ethe anayetakiwa nchini Marekani kushtakiwa kwa mauaji ya mpenziwe, ataendelea kukaa katika gereza la Industrial Area hadi pale atakapomteua wakili wa kumtetea.

Inadaiwa alitorokea nchini Kenya baada ya kumuua Margaret Mbitu.

Bw Kang’ethe ambaye inadaiwa alikwepa kutoka jimbo la Massacheussets mnamo Novemba 2023, alitiwa nguvuni Januari 2024 baada ya Serikali ya Marekani kuomba serikali ya Kenya imrejeshe kufunguliwa kesi ya mauaji.

Baada ya kutiwa nguvuni Bw Kang’ethe alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga lakini akatoroka kabla ya kukamatwa tena katika eneo la Ngong.

Alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyinga, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga aliomba Bw Kang’ethe azuiliwe katika gereza la Industrial Area hadi kusikilizwa na kuamuliwa kwa ombi arudishwe Marekani kujibu mashtaka.

Wiki iliyopita Bw Kang’ethe aliwatimua mawakili Antony Kago na David Muthama kisha akamsihi Bw Onyina ampe muda amtafute wakili mwingine.

Kumwajiri wakili mwingine

Mshukiwa huyo anayetakiwa kufikishwa katika mahakama ya Boston, aliomba aruhusiwe kumwajiri wakili mwingine akidai “tangu Januari sijapata kutetewa kwa njia itakikaniwayo na mawakili wangu na sasa naomba nipewe fursa nimtafute wakili mwingine.”

Mshukiwa huyo alieleza atachukua muda mrefu kumpata wakili mwingine kwa vile polisi walichukua simu yake na hawajamrudishia ndipo apate fursa ya kuwasiliana na wakili mwingine.

“Siwezi kumpigia simu wakili yeyote kwa vile simu yangu ilitwaliwa na polisi na wamekataa kunirudishia nipate fursa ya kuwasiliana na jamaa wangu na wakili vilevile,” Bw Kang’ethe alimweleza hakimu.

Na wakati huo huo, DPP alieleza nakala za ushahidi utakaotegemewa nchini Marekani zimewasilishwa mbele ya mahakama kuhojiwa kubaini ikiwa uko na mashiko kisheria.

Endapo ushahidi huo utapatikana na uwe unamlenga Bw Kang’ethe, basi atakabidhiwa maafisa wa polisi wa Inter-Pol kumsafirisha hadi mahakama kuu mjini Boston kujibu mashtaka ya kumuua Margaret.

Endapo ushahidi huo hautamtambua Bw Kang’ethe kama aliyehusika na kifo cha Margaret, basi ataachiliwa huru.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwa DPP kupitia Wizara ya Mashahuri ya Kigeni, serikali ya Marekani ilisema polisi wake wamekamilisha uchunguzi na “kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia shtaka la mauaji Bw Kang’ethe.”

DPP Ingonga alimweleza Bw Onyina mnamo Jumanne kwamba amekamilisha kuandaa ushahidi utakaotegemewa katika kesi ya mauaji inayomkabili Bw Kang’ethe nchini Marekani.

Kufuatia hitilafu za kumsaka wakili, mahakama ilielezwa huenda kukamilishwa kwa zoezi la kuwasilisha ushahidi mbele ya Bw Onyina kukachukua muda.

Mawakili Kago na Muthama

Lakini familia ya marehemu ilidai kwamba kuwafuta mawakili Kago na Muthama na kutaka muda kumtafuta wakili mwingine ni “mbinu za Kang’ethe za kuchelewesha kurejeshwa kwake nchini Marekani kujibu mashtaka ya kumuua Margaret .”

Muringa Njoroge ambaye ni binamuye marehemu, akizugumza na Taifa Leo alisema “niliona mwili wa marehemu. Alikuwa na majeraha mabaya ungedhani ameraruriwa na mnyama wa porini.”

Binamu huyo alisema mwendazake alikufa kifo cha uchungu.

Bw Kang’ethe alirudishwa katika gereza la Industrial Area hadi Machi 13, 2024, atakaporudishwa kortini kupata maagizo zaidi naye kueleza ikiwa atakuwa amempata wakili wa kuendelea na kesi.

Bw Kang’ethe anapinga kurudishwa Marekani kushtakiwa kwa mauaji ya Margaret, kisa ambacho inadaiwa kilitekelezwa mnamo Novemba 2, 2023.

Polisi wa Marekani walisema Bw Kang’ethe aliifungia maiti ya Margaret ndani ya gari aina ya Toyota Venza na kuliegesha katika garaji kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Boston alipokuwa akifanya kazi kama Mhadisi kisha akatoroka.

Bw Kang’ethe alitiwa nguvuni akijiburudisha katika kilabu kimoja jijini Nairobi mwezi Januari 2024.