Habari za Kitaifa

Alama nyingi za ‘E’ zauma roho viongozi Bonde la Ufa

March 2nd, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

KITENDAWILI sugu cha watahiniwa wa KCSE 2023 kupata alama ya E katika mtihani wa kitaifa kingali kero kwa viongozi kutoka Kaunti ya Uasin Gishu.

Kinaya ni kwamba matokeo hayo yalitolewa katika kaunti iyo hiyo katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi -Eldoret ambayo ndiyo shule ya kipekee ya kitaifa katika kaunti hiyo.

Ripoti ya mwisho ya tathmini ya Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Uasin Gishu imethibitisha kuwa watahiniwa 318 kutoka kaunti hiyo walipata alama ya E.

Kufuatia matokeo hayo ya kutatanisha, viongozi kutoka kaunti hiyo wameratibiwa kufanya mkutano wa dharura ili kujadili hali ya viwango vya elimu katika kaunti hiyo.

Wakiongozwa na Gavana Jonathan Bii, viongozi hao walisema mkutano huo unatarajiwa kuchunguza sababu za matokeo duni katika KCSE mwaka jana kwa lengo la kubaini na hatua za kurekebisha hali hiyo.

Viongozi hao walielezea wasiwasi wao kuwa wengi wa watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana walifeli na hawawezi kuendelea na masomo zaidi hadi vyuo vikuu au kupata kazi za kuridhisha nchini.

“Inafedhehesha kwamba licha ya kuwa kaunti nambari moja nyumbani kwa Rais wa Tano William Ruto, tulitoa alama nyingi za “E” katika mtihani wa KCSE wa mwaka jana,” alishangaa Bw Bii.

Mbunge wa Moiben Phylis Bartoo alisema viwango vya masomo katika shule za za upili vinashuka na kwamba kama viongozi waliochaguliwa wana wajibu wa kushughulikia suala hilo.

“Ni aibu kwa kaunti ya Rais kutoa idadi kubwa ya wanafunzi wenye alama ya E katika mtihani wa KCSE wa mwaka jana na ndiyo maana tumeitisha mkutano wa dharura kujadili suala hilo,” akaongeza Bi Bartoo.

Mwenzake wa Kesses Julius Ruto pia alielezea wasiwasi wake kuhusu alama duni zilizopatikana na kaunti hiyo na kutaja hali  hiyo kuwa ya kutatanisha.

Gavana Bii alisema mkutano wa kujadili suala hilo utakaofanyika hivi karibuni utahudhuriwa na Oscah Sudi,(Kapseret) Phylis Bartoo (Moiben), Julius Ruto (Kesses), Samuel Chepkonga (Ainabkoi), David Kiplagat (Soy) Janet Sitienei (Turbo) Seneta Jackson Mandago na mbunge mwakilishi wanawake Gladys Boss Shollei.

Kulingana na Bw Bii, mkutano huo pia utaleta walimu wakuu na wasimamizi wa bodi za wenyeviti wa bodi, wawakilishi wa wazazi, wasomi na maafisa kutoka Chama cha Kitaifa cha Walimu KNUT na chama chama walimu shule za upili KUPPET tawi la Uasin Gishu.

Haya yanajiri baada ya wazazi waliokuwa na ghadhabu kutoka shule ya upili ya St Martin Mafuta eneo bunge la Soy kumfukuza mwalimu mkuu wa shule hiyo miezi miwili iliyopita kutokana na matokeo duni ambapo shule hiyo iliandikisha matokeo duni.

Shule hiyo iliandikisha alama ya wastani ya E huku mwanafunzi bora akipata alama ya D+.