Wakenya kusubiri kibwagizo cha hotuba za Ruto
NA MWANGI MUIRURI
TANGU nchi ijinyakulie uhuru, Wakenya wamezoea matamshi ya marais wao yenye uzito yanayobadilika kuwa kibwagizo cha hotuba zao na kwa sasa mjadala ni kuhusu iwapo Rais William Ruto naye atarithi mtindo huo.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa Prof Ngugi Njoroge, hali hii imekuwa ni sarakasi n ambazo raia wenyewe wamekuwa wakishabikia si haba kwa kuwa hujihisi wametumbuizwa.
Rais mwanzilishi wa taifa, Mzee Jomo Kenyatta alikuwa mwepesi wa kurusha kibonge cha neno kwa Wakenya ambao alichukulia kama waliomgadhabisha, katika jamii au kisiasa.
“Rais Kenyatta alikuwa mwepesi wa kuachilia fataki la maneno mazito kwa waliomsinya hasa kisiasa na mengi ya majina aliyotumia hayawezi yakachapishwa kwa kuwa yatakera wengi.
“Lakini nyakati hizo kulikuwa na uwiano wa wengi kwamba majina hayo yalisisimua,” asema aliyekuwa afisa wa utawala katika serikali hiyo Bw Joseph Kaguthi.
Bw Kaguthi aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “mimi nimekuwa katika serikali hizi zote na nilikuwa katika huduma ya kutii marais wote.
Bw Kaguthi anasema kwamba “maneno ya Mzee Kenyatta ya kusuta watundu yalikuwa yameegemea Uswahili sana na pia undani wa mila za Agikuyu ambapo kujieleza vizuri, haupitii njia za mkato na maneno”.
Alisema kwamba viwango vya ustaarabu hadi mwaka wa 1978 ambapo Rais Kenyatta aliaga dunia, havikuwa vimeimarika na pia teknolojoia za kimawasiliano hazikuwa zimeimarika jinsi ilivyo leo ambapo lugha hasi huadhibiwa mitandaoni.
Mzee Daniel Moi alirithi mikoba ya uongozi mwaka wa 1978 na akawa naye akitumia majina kama nyang’au (fisi) na kinyang’arika kusuta waliomdhihaki.
Maneno hayo ya marais yamekuwa kivutio kikuu katika mikutano yao ambapo hata yamehifadhiwa katika kumbukumbu za fasihi na huwa yanarejelewa kuadhimisha awamu muhimu za kihistoria hasa katika kuadhimisha siku za kitaifa.
Wakati Rais Mwai Kibaki alichukua hatamu za uongozi kuanzia mwaka wa 2002, alizidisha sarakasi akihudumia Wakenya kwa kuzindua majina kama “pumbavu na mavi ya kuku” dhidi ya waliomkera.
Rais Kibaki aidha alitumia msemo “watu kama hao hawana umuhimu wowote na wanafaa tu kutwangwa makofi”.
Rais Uhuru Kenyatta alichukua hatamu za uongozi mwaka wa 2013 na akachukua mfano wa watangulizi wake, ambapo alizindua maneno kama washenzi, mikora (majambazi) na Kimundu Kiguruki (mwendawazimu) kusuta mahasidi.
Katika hali zote za hotuba za marais hao wote, waliokuwa wakihudhuria mikutano yao walikuwa wakionekana kungojea kwa hamu kuu awamu ambapo rais angetumia maneno ya kejeli.
Mwenyekiti wa baraza la wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago anasema kwamba wafalme wana uhuru wa kusuta walio chini yao hata kwa matusi wanapokerwa na wao.
“Katika uongozi, kuna kukubalika kwa kejeli kutoka kwa wafalme, bora tu yametolewa kwa nia njema ya kuelezea hisia za kero na pia busara ya kukosoa,” akasema.
“Kejeli ya mfalme sio kero bali ni busara ya kukosoa,” asema.
Inatarajiwa kwa hamu kuu Rais Ruto naye azindue kibwagizo cha hotuba zake kwa Wakenya.