Makala

Wakenya wamkumbuka ‘Mr Ibu’ kwa ucheshi wake

March 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

DUNIA inapoendelea kumwomboleza mwigizaji maaarufu kutoka Nigeria, John Okafor, maarufu kama ‘Mr Ibu’, Wakenya watamkumbuka kwa ucheshi mkubwa alioonyesha kwenye senema alizoigiza.

Mr Ibu alifariki Jumamosi, Machi 2, 2024 katika hospitali moja jijini Lagos, alikokuwa akipokea matibabu, kulingana na taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari nchini Nigeria.

Marehemu alikuwa na umri wa miaka 62.

Kiongozi wa Baraza la Waigizaji nchini Nigeria (AGN), Emeka Rollas, alithibitisha kifo chake.

“Ni siku ya masikitiko makubwa kwa Baraza la Waigizaji la Nigeria. Mr Ibu alifariki baada ya kukumbwa na mshtuko wa moyo, kulingana na meneja wake wa muda wa miaka 24, Bw Don Single Nwuzor. Baada ya kukumbwa na hali hiyo, Bw Ibu alizidiwa. Tunamwomba Mungu aiweke nafsi yake mahali pema peponi,” akasema Bw Rollas.

Ingawa kifo chake kimewaacha wengi kwa majonzi, Wakenya, hasa kwenye mitandao ya kijamii, walikuwa wakitumia baadhi ya sehemu za ucheshi kwenye senema tofauti alizoigiza kujiburudisha au kuzua ucheshi mitandaoni.

Baadhi ya senema ambayo imekuwa ikirejelewa sana ni ‘Mr Ibu and Paw Paw’ (yaani Bw Ibu na Papai).

Kwenye senema hiyo, Mr Ibu anataniana sana na mwanawe, Osita Iheme (mwigizaji mwingine maarufu).

Taswira ya senema hiyo ni katika kijijini. Wawili hao wanakemeana kuhusu masuala madogo madogo sana, kwa mfano kuhusu ikiwa papai ni tunda au la.

“Hili ni tunda ama si tunda?” anauliza Mr Ibu kwa mwigizaji Iheme.

“Hili si tunda. Hili ni jiwe!” anasema Iheme, akirejelea ngozi ngumu ya tunda hilo.

Kando na hayo, Wakenya wamekuwa wakitumia baadhi ya picha zake za kuwafananisha baadhi ya watu maarufu kama vile wanasiasa katika hali ya kicheshi (maarufu kama memes).

Wengine pia wamekuwa wakibadilisha sauti katika baadhi ya senema alizoigiza, ambapo baadaye huwa wanaziweka kwenye mitandao ya kijamii kama vile Tiktok.

Marehemu amekuwa akikumbwa na matatizo ya mgando wa damu katika mguu wake kwa miezi kadhaa. Hali hiyo ilimfanya kukatwa mguu huo.

Oktoba 18, 2023, mwigizaji huyo alirai mashabiki wake kumwombea kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimkumba. Pia aliwaomba kumsaidia kifedha.

Novemba 6 mwaka uliopita, familia yake ilitangaza kwamba mmoja wa mguu wake ulikatwa, baada ya kufanyiwa upasuaji mara saba.

Pia, Desemba 17, familia yake ilisema hangeweza kwenda ughaibuni kupata matibabu zaidi, kwani madaktari walisema “hakuwa katika hali nzuri kiafya kusafiri kwa ndege”.

Marehemu ameigiza katika zaidi ya senema 200.

Baadhi ya senema hizo ni Mr Ibu (2004), Mr Ibu and His Son, Coffin Producers, Husband Suppliers, International Players, Mr Ibu in London (2004), Police Recruit (2003), 9 Wives (2005), Ibu in Prison (2006), Keziah (2007) kati ya zingine.

Baadhi ya waigizaji na wacheshi maarufu nchini walisema kuwa kifo chake ni pigo kubwa kwa sanaa barani Afrika.

“Nilikuwa nikimtazama Mr Ibu tangu utotoni wangu. Yeye ndiye alinishawishi kuwa mcheshi,” akasema Njogu Comedian, ambaye ni mwigizaji na mcheshi maarufu kwenye senema nyingi za lugha ya Kikikuyu.

“Ni pigo kubwa kwa tasnia ya uigizaji. Mungu aipe nguvu familia yake,” akasema Bw John Musyoka kwenye mtandao wa ‘X’.