Habari za Kitaifa

Bonge la muungano wa Raila, Ruto na Mudavadi

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA JUSTUS OCHIENG

USHIRIKIANO kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio Raila Odinga unaweza kubadilisha siasa za nchi na kufanya muungano mpya kuchipuka kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 utakaowaleta pamoja vinara hao na washirika wao kutoka Nyanza, Magharibi na Rift Valley.

Rais Ruto ameashiria hadharani ushirikiano wake na kiongozi huyo wa upinzani, akisisitiza kuwa kuna haja ya kukumbatia Wakenya wote bila kujali mirengo yao ya kisiasa.

Tayari, dalili za uhusiano huo zilionekana wabunge kadhaa wa ODM walipojitokeza kumkaribisha rais katika kongamano la Kimataifa la Uwekezaji Kaunti ya Homa Bay huku kiongozi wa nchi akitambua uwepo kwao.

“Nimefurahi leo wabunge ambao wamekuwa wakikwepa mikutano yangu hapa wamejitokeza na hii ni ishara zuri,” Rais alisema.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kitaifa la Azimio Wycliffe Oparanya, ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM, anasema ingawa hakuna mpango wa ushirikiano wa kisiasa na Rais Ruto kwa sasa, hawawezi kupuuza uwezekano wa miungano mipya kuibuka kabla ya uchaguzi wa 2027.

“Mimi ni naibu kiongozi wa chama cha ODM na tunashauriana sana na kiongozi wa chama changu (Bw Odinga). Kwa sasa, Azimio iko sawa, lakini kumbuka pia kwamba hakuna muungano ambao umeshiriki uchaguzi mara mbili ukiwa ulivyokuwa awali,” Bw Oparanya alisema, akiashiria uwezekano wa muungano mpya.

“Kwa hivyo kuna uwezekano kwamba mazingira ya kisiasa yanaweza kubadilika. Hauwezi jua kitakachotokea siku zijazo,” Bw Oparanya aliongeza.

Bw Odinga aligombea urais 2013 kwa tikiti ya Muungano wa Mageuzi na Demokrasia (Cord), kabla ya kuvunjwa kuelekea uchaguzi wa 2017 ambao Bw Odinga aliwania kwa tikiti ya National Super Alliance (Nasa).

Katika uchaguzi mkuu wa 2022 alitumia muungano wa Azimio na kushindwa na Rais Ruto.

Ingawa mbunge wa Homa Bay Mjini Opondo Kaluma anasema kuwa watu hawafai kutarajia mengi kati ya usuhuba wa Ruto na Raila, wadadisi wanasema kuna uwezekano viongozi hao wakaungana kabla ya 2027 ilivyokuwa 2002.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Mark Bichachi anasema “ukweli ni kwamba hatua ya Raila kugombea nafasi ya AU imebadilisha kabisa siasa za Kenya,” Bw Bichachi anasema.

Wachambuzi wengine wa siasa wanasema kuwa kwa kuwa mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi ataongoza kampeni za azma ya Raila kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) kuna uwezekano wa kuibuka kwa muungano wa vigogo wa kisiasa kutoka Magharibi na Nyanza sawa na ilivyokuwa 2007 ulioleta pamoja Ruto, Odinga na Mudavadi.

Watatu hao, miongoni mwa viongozi wengine; waliokuwa Mawaziri Mawaziri Najib Balala, marehemu Joseph Nyaga na baadaye Charity Ngilu walikuwa wanachama wa baraza kuu ya ODM iliyofahamika kama Pentagon.

Profesa Macharia Munene wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika anasema kwamba umoja unaoonekana wa rais Ruto, Bw Odinga na Bw Mudavadi, ni Pentagon mpya.

Prof Munene anahoji kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anaweza kuwa mwathiriwa mkuu iwapo muuungano wa Magharibi utaibuka tena, akiongeza kuwa rais aliposema atahakikisha kwamba wote watakuwa katika serikali, alikuwa akipuuza ‘kauli ya Gachagua kwamba serikali ni ya wenye hisa.’

Kulingana na Bw Herman Manyora, mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, ‘ni dhahiri kwamba kuna makubaliano kati ya Raila na Ruto.’

“Hii inatokana na maslahi ya kisiasa na shinikizo kutoka nje. Hatimaye kutakuwa na muungano,” asema Bw Manyora.

Anaongeza kuwa muungano wa Ruto-Raila bila shaka utakuwa kwa kuwafaa wawili hao binafsi wakijihakikishia nyadhifa zao.

Rais Ruto ameshikilia kuwa kupitia muungano wa kisiasa wa 2007 alimsaidia Bw Odinga kupata wadhifa wa Waziri Mkuu

“Si mnajua hata mimi nilikuwa ODM siku moja, si mnajua hata mimi nilikuwa mtu wa baba, lakini si mnajua siku hizi kwa sababu mimi ni rais, baba amekuwa tena mtu wangu, sasa shida iko wapi? Si maneno ni namna hiyo,” Rais Ruto alisema alipozuru Nyanza.

Aliendelea: “Unajua nimempigia kura Agwambo (Bw Odinga), hata hivyo hajawahi kunipigia kura. Sasa namngoja 2027, kwa sababu ikiwa hatagombea, nitashindana na Kalonzo (Musyoka).