Habari za Kitaifa

Jinsi ndege mbili zilivyogongana jijini

March 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

DANIEL OGETTA Na KEVIN CHERUIYOT

HUENDA marubani wa ndege zilizogongana Jumanne jijini Nairobi walipuuza maagizo ya waelelekezi wa ndege au hawakupata maelekezo kutoka kwa wataalamu hao kwa wakati ufaao.

Kulingana na wataalamu waliozungumza na Taifa Leo, kuna uwezekano kuwa sababu hizo mbili ndizo zilizosababisha ajali hiyo.

Huku uchunguzi ukiendelea kubaini kiini halisi cha ajali hiyo, wataalamu na wadau walisema kuwa huenda tukio hilo likaipaka tope sekta ya uchukuzi wa ndege nchini, inayosifika kutokana na hali yake nzuri.

Uchunguzi huo unaendeshwa na wataalamu wa safari za ndege pamoja na Mamlaka ya Uchukuzi wa Ndege Kenya (KCAA).

Wachunguzi wa KCAA walisema kuwa watafanya uchunguzi kamili wa kinasa sauti na matukio yote yaliyofanyika baada ya ndege hizo mbili kupaa angani.

Mojawapo la masuala ambayo wachunguzi wataangalia, ni sababu ya ndege hizo kupaa zikiwa zimekaribiana sana, na ikiwa marubani walikuwa wakifuata kanuni zilizowekwa za uendeshaji ndege au la.

Wataalamu walisema kuwa hata ikiwa ajali za ndege huwa zinafanyika, hilo ni tukio nadra.

Kulingana na nahodha Nick Ng’ethe anayeendesha Kituo cha Utoaji Mafunzo ya Uendeshaji Ndege cha Samanthair, ajali za ndege kugongana angani huwa tukia nadra sana.

Alisema kuwa ajali hiyo ingeepukwa. Alieleza wale wanafaa kulaumiwa ni usimamizi wa uwanja wa ndege na shule ya mafunzo ya uendeshaji ndege ambayo ndege yake ilihusika kwenye ajali hiyo.

Alisema kwamba KCAA ingehakikisha njia iliyokuwa ikifuatwa na ndege iliyokuwa ikielekea Diani hamkua na ndege nyingine.

Vielekezi vya kufikia afisi za kampuni ya ndege za Safarilink mnamo Machi 5, 2024. PICHA | BONFACE BOGITA