Habari za Kitaifa

Rais Ruto apiga makofi badala ya kutikisa mguu

March 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto Jumanne aliomba msamaha kwa kuvunja sheria na kanuni za bunge licha ya kwamba amewahi kuhudumu kama mbunge kwa miaka 15.

Hii ni wakati alipofungua rasmi kikao cha pili cha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) katika ukumbi wa Bunge la Kitaifa, Nairobi.

Rais Ruto aliwachekesha wabunge hao alipofichua kuwa wakati Spika wao Joseph Ntakirutimana alipokuwa akihutubu, alijipata akipiga makofi, kinyume na sheria za bunge.

“Wakati wa kumpongeza spika ulipowadia nilijipata nikipiga makofi ilhali nilipaswa kujua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kanuni za bunge. Sheria inawahitaji wabunge kupiga sakafu kwa nyayo zao wanapofurahishwa na chochote,” Dkt Ruto akasema.

Rais Ruto alikuwa ameitwa na Spika Ntakirutimana kutoa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho alipochukua fursa hiyo kwanza kuomba msamaha, hali ambayo wabunge hawakutarajia.

“Bw Spika, nachukua fursa hii kuomba msamaha kwa sababu sijakuwepo bungeni sasa kwa zaidi ya miaka 10. Hii ndio maana nimejipata nikikosea,” akasema.

Rais Ruto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Eldoret Kaskazini mnamo 1997.

Alihudumu kwa miaka 15 hadi 2013 alipochaguliwa kuwa Naibu Rais baada yake na Rais Uhuru Kenyatta kushinda katika uchaguzi mkuu. Kwa sasa Bw Kenyatta ni Rais mstaafu.