Habari za Kitaifa

JSC yashusha bakora kwa jaji Kullow, hakimu Wambugu

March 6th, 2024 1 min read

NA SAM KIPLANGAT

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) imemtaka Rais William Ruto kuteua jopo la kumchunguza jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Mohammed Kullow kwa madai ya kuwa mzembe na pia kuwa na utovu wa nidhamu.

Jaji Kullow anayeishi Migori, anashtakiwa kwa kukosa kutoa hukumu na maamuzi katika kesi 116 zilizo mbele yake.

“Tume imemwomba Mheshimiwa Rais kuteua jopo kwa mujibu wa matakwa ya Kipengee 168 (4) na (5) cha Katiba,” Jaji Mkuu Martha Koome, ambaye ni mwenyekiti wa JSC, alisema katika taarifa.

Wakati huo huo, JSC imeafikia uamuzi wa kumfuta kazi Hakimu Mwandamizi Patrick Wambugu kwa utovu wa nidhamu.

Tume hiyo ilisema Bw Wambugu alishtakiwa kwa kubadilisha masharti ya dhamana kinyume cha sheria na kusababisha kuachiliwa kwa mshtakiwa ambaye alikuwa ameshtakiwa kwa kumchafua mtoto wa umri wa miaka sita.

Mshukiwa huyo hajafika mahakamani tangu wakati huo.

Kuhusu jaji Kullow, JSC ilisema maombi matano yaliwasilishwa kutaka aondolewe madarakani na baada ya kusikiliza malalamishi hayo, tume iliridhika kwamba malalamishi matatu kati ya hayo, yalitoa sababu za kuondolewa kwa jaji huyo.

“Tume iliridhika kuwa malalamishi matatu kati ya matano pamoja na hoja ya Tume yenyewe, ni sababu za kumwondoa jaji Kullow kutoka afisini kwa utovu wa nidhamu uliokithiri, uzembe na ukiukaji wa Kanuni za Maadili ya Idara ya Mahakama,” JSC ilisema kwenye taarifa hiyo.

JSC ilisema kuwa kesi iliyowasilishwa na JSC yenyewe ilifichua sababu za kumwondoa jaji huyo afisini kwa sababu ya utovu wa nidhamu, uzembe na ukiukaji wa Kanuni za Maadili katika tume hiyo.