Moses Kuria amezea mate umaarufu wa Raila
NA WANDERI KAMAU
WAZIRI wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, ameonyesha wazi kwamba anatamani sana kuwa na umaarufu alio nao kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga.
Bw Kuria alisema kuwa ingawa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) utafanyika Februari 2025, Bw Odinga atakuwa akijadiliwa katika majukwaa mbalimbali kwa karibu mwaka mmoja, hali itakayodumisha na kuimarisha sana umaarufu wake wa kisiasa.
Kwenye ujumbe alioandika katika mitandao ya kijamii ya Facebook na X (zamani Twitter) mnamo Jumanne, Bw Kuria alitaja suala hilo kama litakalompa “umaarufu mkubwa Bw Odinga bila kufanya lolote”.
“Shughuli ya kumpigia kura yule atakayehudumu kama Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) itafanyika Februari 2025. Lakini kwa mwaka mmoja ujao, mtakuwa mkimjadili Bw Odinga. Ninatamani sana nikiwa mkubwa, niwe kama ‘Baba’[Bw Odinga],” akasema Bw Kuria.
Kauli yake inajiri huku juhudi za kumpigia debe kigogo huyo wa siasa za upinzani kuwania nafasi hiyo zikiendelea kushika kasi.
Juhudi hizo zimekuwa zikiongozwa na Rais William Ruto.
Mnamo Jumanne, Rais Ruto alisema kuwa viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekubali kumuunga mkono mwaniaji mmoja.
Rais Ruto alisema kuwa viongozi hao wamepitisha kauli ya pamoja kumuunga mkono Bw Odinga kuwania nafasi hiyo.
Akihutubia kikao cha kufungua Bunge la Afrika Mashariki (EALA) jijini Nairobi mnamo Jumanne, Rais Ruto alisema hatua hiyo italisaidia bara la Afrika kupata ushindi katika majukwaa mbalimbali duniani.
“Kama mnavyojua nyote, muhula wa mwenyekiti wa AUC Moussa Faki uko karibu kukamilika. Ni zamu ya Afrika Mashariki kuchukua nafasi hiyo,” akasema Rais Ruto.
Tayari, serikali imesema kwamba itafanya kila iwezalo kumpigia debe Bw Odinga kuchukua nafasi hiyo.