Habari za Kaunti

Hatima ya Dkt Monda kuamuliwa na kamati maalum ya Seneti

March 7th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI 

SPIKA wa Seneti Amason Kingi ameteua kamati maalum ya maseneta 11 kuchunguza ripoti kutokana na hoja iliyopitishwa na madiwani wa Kisii ikipendekeza kung’atuliwa afisini kwa Naibu Gavana Dkt Robert Monda. 

Kamati hiyo inajumuisha maseneta sita wanaowakilisha kaunti zao na wengine watano maalum walioteuliwa na vyama tofauti.

Maseneta waliopigiwa kura ni Seki Lenku Ole Kamar (Kajiado), Wafula Wakoli (Bungoma), Joe Nyutu (Murang’a), Ekomwa Lomenen (Turkana), Okiya Omtatah (Busia) na Issa Juma Boy (Kwale).

Maseneta maalum watakaokaa kwenye vikao hivyo ni Maria Sheikh Omar, Profesa Magret Kamar, Beth Syengo, Shakila Abdallah, na Crystal Asige.

Watunga sheria hao wana siku 10 kufanya vikao vya kumhoji Dkt Monda na madiwani waliofanikisha hoja hiyo.

Watawasilisha ripoti kuhusu uchunguzi wao kwa maseneta wote mara watakapokamilisha kibarua kilichoko mbele yao.

Madiwani wa Kisii walimng’atua afisini mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache baada ya kupiga kura 53 za kuunga mkono hoja huku 15 pekee wakipinga.

Walimtuhumu Dkt Monda kwa matumizi mabaya ya mamlaka na sababu nyingine tatu.

Hoja ya kung’atuliwa kwa Dkt Monda iliwasilishwa katika Bunge la Kaunti ya Kisii na diwani wa Ichuni Wycliffe Siocha.

Baada ya kutoa ripoti yao ya uchunguzi katika Seneti, maseneta watapiga kura itakayoamua hatima ya Dkt Monda.

Ikiwa maseneta hao watakubaliana na kung’atuliwa kwa Dkt Monda jinsi walivyofanya madiwani, basi Naibu Gavana huyo atapoteza kiti chake.

Ikiwa watatupilia mbali tuhuma dhidi ya Dkt Monda, atarudi kazini katika wadhifa wake.

Kinyang’anyiro kikali kinatarajiwa katika Seneti wakati wa kumjadili Dkt Monda kwani inatarajiwa pakubwa kwamba mjadala huo utachukua mkondo wa kisiasa baina ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio La Umoja-One Kenya.

Gavana wa Kisii ni Simba Arati.

Kabla ya hoja hiyo kujadiliwa alijaribu kuwarai madiwani waachane nayo lakini wakamkaidi.