Niliporushwa kwa kinywa cha mamba kisiasa wanawake walisimama nami – Ruto
NA MWANGI MUIRURI
RAIS William Ruto amefichua ni kwa nini yeye katika siasa zake huonekana kama wa kupendelea wanawake.
Katika matamshi ambayo huenda yawape mabunge ya Kaunti ambayo magavana ni kinamama ujumbe fiche kwamba hata wawang’atue atasimama nao, Rais Ruto amekiri kwamba huvutiwa nao.
Tayari, Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru ameng’atuliwa mara mbili na bunge lake la Kaunti ya Meru lakini katika bunge la Seneti kukiibuka mkono fiche ulio na misuri ukimkinga asitumwe nyumbani.
Sasa, Rais Ruto amefichua kwamba kwa kawaida hupata wanawake wakiwa waangwana na waaminifu kisiasa.
“Wakati siasa zangu zilikumbwa na msukosuko mkuu kati ya 2018 na 2022, wengi wa wanasiasa ambao walisimama nami kwa dhati ni wanawake,” akafichua.
Tayari, katika eneo la Mlima Kenya, Naibu wa Rais Bw Rigathi Gachagua amefichua kwamba kati ya wanasiasa sita ambao walizindua ukaidi dhidi ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta aliyetaka eneo hilo limpigie kura Raila Odinga, waanzilishi walikuwa mbunge wa Naivasha Jane Kihara na Waziri wa Ardhi Alice Wahome.
Rais Ruto katika hotuba aliyotoa Alhamisi katika kongamano la kusaka ushirikishi wa wanawake katika uongozi, alisema kwamba anajua “katika kura ya urais ya 2022 wengi wa walionipigia kura walikuwa ni wanawake”.
Aidha, alisema kwamba mkondo wake wa kisiasa hadi kufika ikulu wengi wa walioamwamini na wakampa Imani kwamba ndoto zake zingetimia walikuwa wanawake.
Alisema kwamba katika kampeni za kusuka muungano wake wa uwaniaji alistushwa na maamuzi ya Gavana wa Kirinyaga na mwenzake wa Embu Bi Cecily Mbarire ya kubakia katika mrengo wake.
“Ilikuwa ni awamu ngumu na hasi lakini maamuzi yao licha ya taswira kuangazia kinyume, ya kubakia nami yalinidihirishia ujasiri wa kipekee na ambao ni lazima nami niutunze,” akasema.
Rais Ruto pia alisema msukumo wake wa kuunga wanawake mkono hutokana na hali kwamba familia yake iko na wanawake wengi kuwaliko waume.
Katika familia yake ya watoto Saba akiwa na mama wa taifa Bi Rachel, wanawake ndani ya hilo boma ni sita kati ya wote tisa.
Rais Ruto alifichua jinsi akisaka kusaidia wanawake wengi kuibuka washindi ndani ya mrengo wake alikuwa akuwapigia simu na kuwapa maelekezo.
“Hasa huyu Gavana wa Nakuru Susan Kihika, nilikuwa nikimwambia kwamba hakuwa na ulumbi wa kuchumbia wapigakura. Nilimwambia kwamba ni lazima angeimarisha mbinu zake ndipo aanze kutesa ulingo wa kisiasa. Na alifaulu na najivunia ufanisi huo,” akasema.
Rais Ruto aliwapa dokezi wanasiasa wa kike kwamba “katika kivumbi cha kampeni usiwe wa kushikilia kuonekana mrembo kwa kuwa uwanja huwa wa msukumano”.
Rais Ruto alishikilia kwamba ni lazima ataendelea kuunga magavana wa kike nchini mkono kwa hali na mali, akiwaahidi hata makuu ya kisiasa katika siku zijazo.