Siasa zatingika Rais Ruto akipendekeza mgombea mwenza awe mwanamke
NA MWANGI MUIRURI
SAUTI ya kiongozi wa nchi katika siasa za Afrika huwa na uzito mwingi na hii ndio sababu wachambuzi wa masuala ya kisiasa tayari wameanza kuichambua kauli ya Rais William Ruto mnamo Alhamisi alipoahidi kwamba mgombea mwenza wake huenda atakuwa mwanamke mwaka 2027.
Licha ya kwamba hakujituma moja kwa moja kutangaza ni lini, Rais Ruto akihutubia kongamano la viongozi wanawake katika hoteli ya Safari Park jijini Nairobi alisema atashauriana na Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu mwelekeo huo.
“Kuelekea huko mbele mimi na Bw Gachagua itabidi tupange na tuelewane vile itakuwa… kwamba ikiwa mwaniaji wa urais ni mwanamume, basi naibu awe ni mwanamke na ikiwa mwaniaji urais ni mwanamke, iwe ni mwanamume katika wadhifa wa unaibu,” Rais Ruto akasema huku akishangiliwa kwa dhati na waliohudhuria kongamano hilo.
Aliongeza kwamba hali hiyo wanafaa kuifanya sheria ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).
“Hili tunafaa tujumuishe pia kwa wadhifa wa ugavana,” akasema kiongozi wa nchi.
Hali iliingia siasa kamili wakati Rais alimsimamisha Gavana wa Embu Cecily Mbarire na akafichua kwamba “haikuwa bahati ama ajali bali ilikuwa hatua ya kimakusudi Bi Mbarire kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha UDA”.
Hayo yakijiri katika hali ambapo Bw Gachagua anapambana kwa kila mbinu kuibuka kama msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya, ufichuzi wa Rais Ruto kwamba yeye mwenyewe alipanga Bi Mbarire aibuke mwenyekiti wa chama kikubwa zaidi ndani ya muungano tawala wa Kenya Kwanza, unazua msisimko wa kisiasa.
Wandani wa Bw Gachagua wakiongozwa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga, Mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi na aliyekuwa mbunge wa Kieni Kanini Kega (mbunge wa EALA) wamekuwa wakiweka wazi wasiwasi wao.
Wao hudai ugumu wa Naibu Rais kukubalika Mlimani huchochewa na nguvu ‘fiche’.
Ni hivi majuzi tu ambapo Rais Ruto aliingilia kati kuwahimiza wandani wa mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kukoma kumdunisha Bw Gachagua hadharani kupitia kumwombea afutwe kazi 2027.
Wakiongozwa na Seneta wa Murang’a Joe Nyutu na mbunge wa Gatanga Edward Muriu, walikuwa wameanza mchakato wa kupigia debe kutemwa kwa Bw Gachagua na Bw Nyoro aorodheshwe katika tiketi ya kuwania urais 2027 Rais Ruto akisaka awamu ya pili na katika mpito wa 2032, mbunge huyo wa umri wa miaka 39 sasa arithi Ikulu.
Licha ya Bw Nyoro kujitokeza na kutangaza kwamba hakuwa na nia ya kumhujumu na kumrithi Bw Gachagua, hotuba ya Rais ya kupendekeza iwe sheria kuhusu mgombea mwenza huenda ichipuze msururu wa siasa za ushindani eneo hilo.
Kwa sasa, eneo hilo la Mlima Kenya liko na wanasiasa wa kike wanaovuma na ambao ni mbunge maalum Sabina Chege, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na kinara wa Narc Kenya Martha Karua ambao pamoja na Bi Mbarire, hupigiwa upatu wa uwezekano wa kuibuka na mnofu wa Ikulu.
Aidha, Rais Ruto katika siku za hivi karibuni ameonekana akiwa na uchumba wa kisiasa na kinara wa upinzani Raila Odinga na ambapo kwa pamoja wawili hao hawafichi kuwa na mapenzi ya dhati ya kisiasa na gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.
Mdadisi wa siasa za Mlima Kenya Prof Ngugi Njoroge alisema kwamba matamshi ya Rais huwa hayachukuliwi kwa mzaha.
“Hii kauli ya Rais kuhusu mgombea mwenza inaashiria maono yake ya hali ya baadaye nchini,” alisema Prof Njoroge.
Alisema kwamba shida kuu ya siasa za Kenya tangu mfumo wa siasa za vyama vingi ukumbatiwe nchini kikamilifu mwaka wa 1992, ni hali kwamba vyama husambaratika na vingine kuchipuka katika kila uchaguzi.
“Hiyo ndio sababu matamshi kuwa UDA itapiga msasa suala la jinsia katika ugombeaji wa urais yanaweza yakadadisiwa kwa udharura wa 2027 ikitarajiwa kwamba huenda nacho kisambaratike 2032,” akasema.
Hata hivyo, alisema kwamba afueni inaweza kuwa Rais kutumia uchaguzi wa 2032 kupisha sera hiyo ya jinsia na Bw Gachagua awe ndiye atawajibishwa kuteua mgombea mwenza wa kike.
“Rais Ruto si mtu wa kutafuna mdomo wakati anapotoa matamshi yake na wale ambao wamekuwa wakifuatilia msukumo wake wa kisiasa, watakiri kwamba yeye huwa muwazi na husema yaliyo moyoni mwake. Hili la mgombea mwenza nawaomba mlipe tu macho na masikio kwa kuwa litazaa mwamko mpya katika awamu isiyo mbali na sasa,” akasema mchanganuzi huyo.